Friday, 11 December 2015

MKUU WA WILAYA YA IRINGA AZITAJA TAASISI NNE ZINAZOCHANGIA KUBOMOA MAADILI, NI PAMOJA NA REDIO FMMKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera amezitaja taasisi nne yakiwemo madhehebu ya dini na vyombo vya habari kwamba baadhi ya mambo wanayofanya yanachangia kumomonyoa maadili ya viongozi wa umma na taifa kwa ujumla.

Kasesera alizitaja taasisi hizo juzi mjini Iringa kwenye mdahalo wa maadhimisho ya siku ya maadili nchini uliondaliwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi Nyanda za Juu Kusini kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Misaada la Watu wa Marekani (Usaid).

Taasisi zingine kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya ni pamoja na vyama vya siasa na wakurugenzi wa halmashauri.

Katika mdahalo huo uliofunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Kasesera alisema; “kwa upande wa vyama vya siasa imekuwa ni jambo la kawaida kuwapata viongozi wake na wale wanaogombea nafasi mbalimbali za uwakilishi wa wananchi kwa kununua kura kwa wapiga kura.”

Masenza alisema nchi haiwezi kupata maendeleo kama itakosa maadili kwani upo ushahidi unaonesha kwamba asilimia 80 ya kila mafanikio yanayotokea duniani chanzo chake ni maadili.

Kasesera alisema nchi haiwezi kupata viongozi bora watakaofanya kazi kwa kuzingatia maadili na miiko mingine ya uongozi kama vyama vya siasa vitaendelea kuwapokea na kuwapigia debe viongozi wanaonunua uongozi.

Kwa upande wa madhehebu ya dini alisema taasisi hizo zimekuwa zikipokea fedha toka kwa wala rushwa, kubariki fedha hizo na wakati mwingine kuwapongeza na kuwapigia debe viongozi wenye tuhuma mbalimbali za rushwa katika jamii.

Kuhusu halmashauri alisema rushwa katika manunuzi na tenda mbalimbali zimewafanya baadhi ya wakurugenzi na watendaji wao kukiuka kwa kiasi kikubwa maadili ya kazi zao ili waendelee kunufaika.

Kwa upande wa vyombo vya habari, Kasesera alisema imekuwa ni jambo la kawaida hasa kwa baadhi ya redio za masafa mafupi (FM) kuendesha vipindi vinavyovunja utu na maadili ya mtanzania.

“Viko vipindi vinavyotangazwa mchana kweupe lakini vingine ni vya usiku. Ukisikiliza unajiuliza swali hivi hizi redio zinapeleka ujumbe gani kwa vijana wetu……yaani kuna vipindi vinawafundisha vijana namna ya kufanya ngono na maneno mazuri ya kutongozana….kweli tunajenga maadili au tunaua maadili?” alisema.

Katibu wa  Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi Nyanda za Juu Kusini, Erick Mbembati alisema ili kuirudisha nchi katika maadili, wameiomba serikali iingize suala la maadili kwenye mitaala ya shule za msingi, sekondari na vyuo.

“Pamoja na kuwepo na mitaala hiyo mashuleni na vyuoni ni muhimu wazazi au walezi wakaacha kuwatumia vijana kwa shughuli za kulea watoto majumbani na badala yake tumie watu wazima, wapo na wanaweza kufanya kazi hiyo kama maslai yao yatazingatiwa,” alisema.

Alisema wafanyakazi wa majumbani vijana kwa upande mwingine wamekuwa chimbuko la uharibifu wa maadili kwa watoto kwasababu ya kukosa hekima na busara.  

Kuhusu vyama vya siasa alisema ni muhimu vikashirikiana na tume yao na Taasisi ya Kupambana na Kupunguza Rushwa (Takukuru) ili visaidiwe kuwafahamu watu wasiofaa kupewa dhamana za uongozi kwasababu ya kukosa maadili.

Mbembati aliyasema hayo baada ya wachangiaji katika mdahalo huo kuuliza sababu za baadhi ya viongozi waliohusishwa katika tuhuma mbalimbali za ufisadi kuendelea kupewa dhamana na vyama vyao za kugombea nafasi mbalimbali na hatimaye wananchi kuwachagua.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment