Tuesday, 22 December 2015

MKUU WA MKOA, MWENYEKITI WA CCM MKOA WA IRINGA NA WAJUMBE WAKE WA KAMATI YA SIASA WAFUNGIWA OFISINI

ZAIDI ya vijana 50 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini, wanaojiita “wafia chama” kwa zaidi ya saa mbili juzi waliwafungia ndani ya ofisi za CCM Mkoa wa Iringa wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo akiwemo Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu wanayeshinikiza aachie ngazi.

Msambatavangu anatuhumiwa na baadhi ya makada wa chama hicho kukihujumu chama hicho jimbo la Iringa Mjini wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu jambo walilosema limesababisha wapoteze kata 14 kati ya 18 na jimbo hilo kwa mara nyingine tena kwa Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).  

Wengine waliokutwa na kadhia hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Elisha Mwampashi, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Dk Yahaya Msigwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Ephraim Mhekwa.

Wengine ni pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahamudu Mgimwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Joseph Muhumba.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyefika kikaoni hapo kwa kuchelewa alijikuta akiingia katika kundi la wajumbe waliofungiwa katika ofisi hizo baada ya kuwaomba vijana hao wafungue geti la kuingilia na kutokea katika ofisi hizo zilizopo ghorofa ya kwanza ya jengo hilo.

Baada ya kufungua geti hilo huku wakimuahidi mkuu wa mkoa huyo kutoondoka katika ofisi hizo mpaka watakapojiua nini kitafanywa na viongozi wa chama hicho kama mwenyekiti wa ccm mkoa wa Iringa hataachia ngazi kwa hiari yake mwenyewe, walifunga tena geti hilo mara tu baada ya mkuu wa mkoa kuingia katika ofisi hizo.

Wakiwa wamefungiwa ndani, makechelo wa Polisi na wale Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa katika gari tatu za polisi aina ya Landlover waliwasili katika ofisi hizo zilizopo jirani na stendi kuu ya mabasi yaendeyo mikoani kwa lengo la kuwadhibiti vijana hao.

Baada ya askari hao kufika vijana waliokuwa na funguo za geti hilo walipandisha harakaharaka ghorofani na kufungua geti hilo kabla Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa na Katibu Mwenezi wake, hawajatoka na kuzungumza nao.

“La kwanza niwapongezeni kwamba mnakipenda chama na mnapenda chama kipate ushindi, pili niwapongezeni mnauchukia usaliti ndani ya chama. Tatu lazima mfahamu kwamba kuna vikao vinapaswa vijadili suala la usaliti, hoja yenu ni ya msingi,” alisema Mwampashi.

Naye Dk Yahaya alisema uongozi wa chama hicho mkoa umepokea taarifa za usaliti toka ngazi ya chini na mchakato wa kuzijadili umeanza na akawaomba vijana hao kama wana nyongeza wawasilishe katika kikao hicho cha kamati ya siasa ya mkoa.

Akizungumzia tuhuma wanazomuhusisha nazo Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa; mmoja wa vijana hao Salum Mbungu ambaye ni Katibu wa Vijana Kata ya Ruaha na Katibu wa Makatibu wa Vijana wa kata zote 18 za jimbo la Iringa Mjini alisema:

“Tunataka Mwenyekiti wa Mkoa ajiuzulu kwa hiari yake, kuna ushahidi tosha unaomuhusisha yeye binafsi na baadhi ya vijana wa CCM kukihujumu chama wakati wa Uchaguzi Mkuu,” alisema.

Mbungu alisema wanao ushahidi unaoonesha kiongozi huyo alikuwa akiwashawishi baadhi ya wana CCM kuwachagua wagombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwasababu alikuwa mpiga debe maarufu wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa wakati akiwa katika mchakato wa kuwania urais kupitia CCM.

Akizungumzia tukio hilo baada ya vijana hao kuombwa kutawanyika huku wakihakikishiwa kwamba hoja zao zinafanyiwa kazi katika vikao husika, Msambatavangu alisema; “tuhuma zinazotolewa na vijana hao na wana CCM wengine dhidi yake sio za kweli, zinalenga kuchafua hadhi yake na kuficha ukweli wa sababu zilizosababisha wapoteze jimbo hilo.”

Alisema tuhuma zinazotolewa dhidi yake ni za kupangwa na zinafanywa na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga kwa maslai yake binafsi ili ashindwe kusimamia shughuli za chama kwa kuzingatia katiba, kanuni na taratibu.

“Mimi siwezi kujiuzulu kwa shinikizo la kikundi cha vijana wanaotumiwa vibaya. Tuna utaratibu wa kufanya tathimini za uchaguzi, kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa; mkoa ukishachambua unapeleka Taifa na maamuzi yanafanyika,” alisema.

Alisema wanaomtuhumu kwamba yeye ni msaliti wanajua sababu nyingi, kwa kuwa zinajulikana, za kwanini walishindwa uchaguzi katika jimbo la Iringa Mjini pamoja na kutumia nguvu kubwa.

Alisema anao ushahidi wa kina na wa kutosha wa jinsi kiongozi mwenzake huyo wa mkoa anavyoratibu mipango ya kumchafua kwa kutumia baadhi ya vijana hao ili kuficha ukweli huo.

“Nataka niwaambie watanzania wazaziwazi kwamba kama mimi nilikisaliti chama eti kwasababu nilikuwa Timu Lowassa hiyo ni hoja ya kipuuzi kabisa. Ndani ya CCM kuna demokrasia inayowapa fursa wanaCCM kumuunga mkono mgombea wanayemtaka, na hiyo hawezi kusababisha sisi tuitwe wasaliti, utaratibu huo upo toka enzi za Nyerere,” alisema.

Alisema wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM, Lowassa aliungwa mkono na zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa halmashauri kuu, zaidi ya wenyeviti 16 wa mikoa na viongozi na wanachama wengine mbalimbali kwasababu demokrasia hiyo inawaruhusu.

Alisema pamoja na Lowassa kuungwa mkono na kundi kubwa alijitoa CCM na kujiunga na Chadema, waliomfuata walikuwa wachache sana na hiyo haina maana kwamba waliobaki CCM ni wasaliti.

“Nimeanza kupigwa vita muda mrefu, na vita hii ilianzia kwenye mchakato wa kupata mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini kwasababu mimi nilikuwa mmoja wa wagombea ambaye nilipigwa vita na baadhi ya viongozi, vita hiyo inaendelea kwakuwa mgombea waliyemtaka ameshindwa na wanafanya hivyo wakitafuta kujikosha kwasababu waliwahakikishia wana Iringa kwamba ni lazima watakomboa jimbo la Iringa Mjini,” alisema.

Alisema amepeleka taarifa makao makuu ya chama ya jinsi anavyohujumiwa na kupakwa matope kwa tuhuma za uongo na kwamba yupo tayari kutoa ushahidi wa kutosha pindi atakapotakiwa kufanya hivyo ili kusafisha jina lake.

“Leo imefika mwisho, nataka niseme kama mwenyekiti niliyechaguliwa na wilaya zote za mkoa wa Iringa; hujuma hizi zisizo na ushahidi, hazivumiliki na zinachosha; nasema kama kuna mtu anatumia uongo, uzushi na majungu kutaka mimi ning’oke, kabla sijang’oka Mungu atajibu,” alisema.

Alisema hatishwi wala haogopi mipango inayofanywa na vijana hao, na hata kama wana mpango wa kumua, wamuue, lakini wajue historia itawahukumu kwasababu kazi anayofanya ya kukijenga chama hicho na nguvu aliyotumia kwenye kampeni za CCM mkoa mzima kwa kutumia rasilimali zake wanazijua.

Alisema inashangaza wanayemuita msaliti (yeye) ilikuwaje wakamvumilia katika kipindi chote cha miezi miwili ya kampeni na kuja kumutuhumu baada ya uchaguzi kufanyika na kupokeza jimbo.

“Inawezekanaje katika miezi miwili ya kampeni, Jesca akaushinda uongozi mzima wa mkoa, uongozi wa vijana, uongozi wa wanawake, uongozi wa wazazi, viongozi na wanachama wa kata na matawi, na akavumiliwa katika kipindi chote hicho, kama hoja hizo sio za kipuuzi,” alisema.


Alisema vijana hao wakiendelea kutumiwa wajue kabisa kwamba hawatakuwa wanafanya kazi ya kukinusuru chama na akawataka wakae chini, watafakari na wajipange upya kwa kutumia ngazi zote za chama kujipanga upya.

Akizungumza kwa njia ya simu na mtandao huu kutoka Ludewa mkoani Njombe, Katibu wa CCM mkoa wa Iringa, Mtenga alikanusha kuhusika na njama zinazodaiwa na mwenyekiti wake huyo.

"Hicho kikao wameitisha wenyewe, mimi sipo Iringa, ninawezaje kuhusika na mambo yaliyokuwa yakiendelea katika kikao walichohitisha wao wenyewe, sitendewi haki na kimsingi sina sababu ya kufanya hayo yanayodhaniwa nayafanya," Mtenga alisema.

Reactions:

1 comments: