Thursday, 3 December 2015

MBUNGE COSATO CHUMI ATOA MSAADA WA VIFAA TIBA HOSPITALI YA WILAYA YA MUFINDIMBUNGE wa Jimbo la Mafinga Mjini lililopo wilayani Mufindi mkoani Iringa, Cosato Chumi ameendelea kuboresha huduma katika hospitali ya wilaya ya Mufindi baada ya juzi kutoa msaada unaojumuisha vitanda vya kisasa 19 vya kulaza wagonjwa, magodoro 11, viti vya kubeba wagonjwa na vifaatiba mbalimbali.

Msaada huo uliomaliza tatizo la vitanda katika hospitali hiyo yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 237 kwa mara moja unakuwa watatu kutolewa na mbunge huyo kijana katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Mbali na msaada huo wa juzi, Chumi kwa kupitia asasi yake ya Mufindi Vijana kwa Maendeleo (MUVIMA) alitoa msaada wa viti 33 vya kubeba wagonjwa na vitanda 27.

“Tuna urafiki na asasi ya kimataifa ya Rafiki Surgical Mission ya Australia, hawa ndio wanaotutafutia vifaa tiba hivi; kazi tunayofanya ni kuwapelekea maombi ambayo kwa kweli yamekuwa yakizaa matunda kila tunapowaomba,” Chumi alisema wakati akikabidhi msaada huo.

Alisema yeye ni mkereketwa wa maendeleo katika jimbo na wilaya hiyo kwahiyo ataendelea kutafuta marafiki wengine ili wasaidie maendeleo ya wananchi wake katika sekta nyingine.

“Lazima tujue kwamba serikali haiwezi kufanya kila kitu, ni lazima kuwepo na nguvu ya wananchi, marafiki na wadau wengine ya kujazia pale penye mapungufu,” alisema huku akipongeza mwanzo katika kushughulikia kero ulioanza kuoneshwa na serikali ya awamu ya tano ya Dk John Magufuli.

Akizungumzia wajibu wa wabunge katika wilaya hiyo, Katibu wa CCM wa wilaya ya Mufindi, Jimson Mhagama alisema; “sio tu katika kuisimamia serikali kutekeleza majukumu yake na kutunga sheria lakini pia ni kufanya kazi za kujitolea kama inavyofanywa na Chumi.”

Akiwa kiongozi wa kwanza wa CCM mkoani Iringa kupongeza kazi iliyoanza kufanywa na serikali ya Dk Magufuli, Mhagama alisema serikali ya CCM kwa kushirikiana na wagombea wake iliahidi kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazowakabili watanzania.

“Nitumie fursa hii kumpongeza sana ten asana mbunge wa jimbo hili jipya la Mafinga Mjini, ndugu yetu Chumi kwa kazi kubwa anayofanya kwa wananchi wa wilaya hii. Amekuwa akishiriki katika maendeleo kabla na anaendelea akiwa mbunge,” alisema.

Akishukuru kwa msaada huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Abdul Msuya alisema hospitali ya wilaya ya Mufindi inapokea wateja 130 kwa siku.

“Baada ya kupokea msaada huu nishukuru kwa kusema mbunge amesaidia kumaliza kabisa ule upungufu wa vitanda tuliokuwa nao, tunachohitaji kwasasa ni taa kwa ajili ya chumba cha upasuaji na mashine ya kufulia,” alisema.

Dk Msuya alisema hospitali hiyo ina upungufu wa wodi za kulaza wagonjwa, madaktari na watoa huduma wengine jambo linalopunguza ufanisi katika utoaji wa huduma zake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment