Wednesday, 30 December 2015

MBUNGE AAHIDI KUTUMIA FEDHA ZA KUNUNUA SHANGINGI KUJENGA VISIMA VYA MAJI KWA WAPIGA KURA WAKE

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood akimtwisha ndoo ya maji bibi Antonia Tebrisi (71) mkazi wa Mtaa wa Lukobe Juu, Manispaa ya Morogoro.

Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Abdulaziz Abood, ameahdi kutumia fedha ambazo wabunge wanakopeshwa kununua magari, kuchimba visima vya maji kuwezesha wananchi wapatao 1,700 wa kata ya Mkundi kupata maji safi na salama.

Maamuzi hayo yanafuatia  kujionea hali halisi ya shida ya maji kwa wakazi hao ambapo amesema  suala la maendeleo ya wananchi wake litapewa kipaumbele cha hali ya juu kwa kushiriki moja kwa moja na kwa kutoa misaada ya vifaa na fedha akishirikiana na viongozi wenzake na wadau wengine .

Abood alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo anataka kuwatumikia wananchi wa jimbo lake kwa kasi zaidi ili kuharakisha maendeleo na upatikanaji wa huduma bora za kijamii zikiwemo za elimu, afya na maji safi na salama.

Alisema katika kutekeleza kaulimbiu ya ‘ Hapa Kazi tu’ , atasaidia upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Mtaa wa Mkundi –CCT , kata ya Mkundi kwa kuchimba visima viwili vya maji.

“Uchimbaji wa kisima kimoja unagharimu zaidi ya Sh milioni 25 na viwili ni zaidi ya Sh milioni 50…hivyo basi nitatumia fedha ambazo wabunge tunakopeshwa kwa ajili ya kununua magari yetu kuchimba visima vya maji ili mpate maji safi na salama, ” alisema Abood.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment