Monday, 28 December 2015

MAWAKILI WA CCM NA CHADEMA WAVUTANA KAMA DESEMBA 9 ILIKUWA SIKU YA KAZI AU PUBLIC HOLIDAYMVUTANO wa kisheria uliohusu Desemba 9 ya mwaka huu kama ilikuwa ni siku ya mapumziko (Public Holiday) au siku ya kazi (Working Day) umeibuka hii leo katika mahakama ya hakimu mkazi Iringa wakati mahakama hiyo ilipokuwa ikisiliza shauri la waliokuwa wagombea udiwani katika kata mbalimbali za Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaoomba wapunguziwe gharama za kusikiliza kesi za kupinga matokeo ya chaguzi hizo.

Katika uchaguzi huo wa Oktoba mwaka huu, wagombea hao walipoteza kata 14 kati ya 18 za jimbo hilo kwa wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kufungua kesi za kupinga matokeo hayo, Novemba 26, mwaka huu.

Kwa mujibu wa sheria, siku 14 baada ya kufungua kesi ya uchaguzi, mdai anaweza kuwasilisha maombi ya kupunguziwa au kusamehewa gharama za usikilizaji wa kesi hiyo kama hana uwezo.

Kwa kesi za udiwani gharama zilizoainishwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ni Sh 500,000 kwa kila mdaiwa jambo linalomfanya kila mdai kulipa Sh Milioni 1.5 kwa wadaiwa watatu ambao ni  Mwanasheria Mkuu wa serikali, Msimamizi wa Uchaguzi na mshindi wa udiwani.

Kwa kupitia wakili wao, Anthony Kanyama baadhi ya wagombea hao wanaiomba mahakama hiyo iwapunguzie kutoka Sh 500,000 hadi Sh 150,000 kwa mdai mmoja.

Mawakili wa upande wa wadaiwa, Happines Flavian ambaye ni wakili wa serikali, Leah Francis wakili wa manispaa na Jane Massey wakili wa kujitegemea wameiomba mahamakama hiyo itupilie mbali ombi la wadai hao kwasababu mbalimbali ikiwemo ya kuwasilishwa ombi hilo nje ya muda ambao ni siku 14 baada ya kufungua kesi ya kupinga matokeo.

Wakili wa serikali, Flavian aliiiambia mahakama hiyo kwambawakati kesi zilifunguliwa Novemba 26, ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo Desemba 10, badala ya Desemba 9 au kabla ya siku hiyo ili mradi zisizidi siku 14.

Wakili wa wadai Kamanya alisema mawakili wa upande wa wadai wanajua kwamba Desemba 9 ilikuwa ni Public Holiday kwa kuwa kwa mujibu wa sheria inayozitambua Public Holiday, Rais hana mamlaka ya kufuta siku hiyo japokuwa anaweza kubadili jambo la kufanya siku hiyo.

Alisema kila mtanzania anajua siku hiyo kwa mujibu wa maelekeo ya Rais ilikuwa ni Public Holiday ambayo watanzania waliitumia kufanya usafi katika maeneo yao na hakuna shughuli za kawaida za serikali na idara zake zilifanyika siku hiyo.

“Na ndio maana mawakili wasomi katika ombi lao la kutaka shauri hili litupiliwe mbali wameshindwa kutoa ushahidi mbele ya mahakama hii kama siku hiyo mahakama hii iliendelea na kazi zake za kawaida, na kama iliendelea na kazi zake za kawaida basi watwambie ni kesi gani zilisikilizwa” Kanyama alisema.

Akitetea kwamba siku hiyo iligeuzwa kuwa siku ya kazi, wakili wa serikali alinukuu Government Notice iliyomnukuu Rais mwenyewe akiitangaza siku hiyo kwamba itakuwa ni siku ya kazi.

“Hata hapa mahakamani tangazo lilibandikwa likiwataka watumishi wote kufika kazin, kufanya usafi na kuendelea na kazi zao kama kawaida. Mimi mwenyewe niliingia kazini kwangu saa 1.30 asubuhi na nilitoka ofisini saa 9.30. Nahakika mahakimu na wafanyakazi wengine wa mahakama hii ni mashahidi,” alisema Flavian na kusisitiza kwamba siku hiyo pamoja na kwamba ni Public Holiday lakini ilikuwa ni siku ya kazi kwa mujibu wa Governement Notice hiyo.

Baada ya kusikiliza mabishano ya pande hizo mbili mahakama hiyo inatarajia kutoa uamuzi wa ombi la wadai hao kesho asubuhi.

Wakati ombi hilo likisikilizwa waliokuwa wagombea ubunge wenye ushawishi mkubwa  katika Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliyeshinda kupitia Chadema na Frederick Mwakalebela anayelalamikia matokeo ya ushindi huo wa Msigwa walikuwepo mahakamani hapo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment