Sunday, 27 December 2015

MAGUFULI NA SHEIN WALIPOKUTANA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM NA KUZUNGUMZIA HALI YA KISIASA ZANZIBAR

Rais  John Pombe Magufuli akizungumza na Rais wa Zanzibar Dk.Shein.

RAIS John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mazungumzo hayo jana, Rais Shein amesema lengo la mazungumzo hayo, ilikuwa kumpa taarifa Rais Magufuli, kuhusu hali ya mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea huko Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu.

Amesema mazungumzo ya hali ya Zanzibar yanaendelea chini ya Kamati Maalumu yenye viongozi wakuu wastaafu na viongozi wakuu wa sasa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo yeye ndiye Mwenyekiti.

Wajumbe Mbali na Dk Shein ambaye ni Mwenyekiti, wajumbe wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

Wengine ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungo wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete. Pia yupo Rais mstaafu wa Awamu ya Sita wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume na Rais mstaafu wa Awamu ya Tano wa Zanzibar Dk Salmin Amour.

Amesema tayari kamati hiyo imeanza mazungumzo tangu Novemba 9, mwaka huu na yamelenga kujadili hatma ya Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, uliofutwa. Rais Shein amebainisha kuwa mazungumzo hayo bado yanaendelea.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment