Wednesday, 16 December 2015

MAADHIMISHO YA SIKU YA BODABODA TANZANIA, YAFANYIKA KITAIFA MJINI IRINGA
WAENDESHA pikipiki (bodaboda) 455 toka wilaya zote za mkoa wa Iringa wamehitimu mafunzo ya wiki moja ya sheria za usalama barabarani na kutunukiwa  vyeti vyao na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, John Kiteve kwenye maadhimisho ya siku ya bodabora Tanzania, yaliyofanyika kitaifa mjini Iringa juzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Benjamin Kuzaga aliwataka wahitimu hao kuwa kichocheo cha madereva wengine kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kumaliza tatizo la ajali nyingi za barabarani zinazochangiwa kwa kiasi kikubwa na udereva usiozingatia sheria.

Akizungumzia takwimu za ajali za bodaboda kwa mkoa wa Iringa ambazo ziliripotiwa katika vituo mbalimbali vya Polisi mkoani hapa kati ya Januari hadi Novemba 14 na kati ya Januari hadi Novemba 2015,  Kuzaga alisema:

“Kati ya Januari hadi Novemba 2014 kulikuwa na ajali za bodaboda 39 na zilizosababisha vifo zilikuwa 19; na kati ya Januari hadi Novemba 2015 kulikuwa na ajali 21 na kati yake zilizosababisha vifo zilikuwa 17,” alisema.

Alisema takwimu hizo zinaonesha kupungua kwa ajali za bodaboda zinazoripotiwa katika vituo vya Polisi jambo linaloongeza matumaini ya kulimaliza tatizo hilo.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, Kuzaga alizungumzia pia wimbi kubwa la wizi wa pikipiki katika mikoa ya nyanda za juu kusini na akawataka wanunuzi kuwa makini wanapohitaji kununua pikipiki kwa watu wasiowafahamu.

Awali Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na utoaji wa mafunzo hayo ya APEC Tanzania, Respicius Timanywa alisema pamoja na umhimu mkubwa wa mafunzo hayo bado kuna mwitikio mdogo kutoka kwa walengwa wanaotakiwa kushiriki.

“Kuna baadhi ya madereva walipata leseni kiujanjaujanja; pamoja na kutojua sheria za usalama barabarani madereva hao hawataki kushiriki mafunzo ya aina hii kwakuwa wanaweza kuendesha pikipiki zao barabarani,” alisema.

Alisema kwasababu pikipiki ndizo zinazoongoza kwa kusababisha ajali nyingi nchini, kuna haja ya kuangalia sheria zilizopo ili kutoa adhabu kali kwa wahusika.

“Kule Rwanda ukikamatwa hujavaa kofia ya kuzuia ajali, adhabu yake ni kifungo cha mwaka mmoja jela. Na sisi tunaweza kuwa na sheria kama hiyo ili kuwabana madereva wa pikipiki wanaokiuka sheria na ambao hawajapata mafunzo,” alisema.

Akizungumzia urasimu wanaokutana nao madereva wa bodaboda wakati wakiomba leseni za udereva, Timanywa aliomba Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) iwatambue na kuwahudumia kwa kasi madereva waliopitia mafunzo kwa utartibu utakaohusisha utambuzi utakaofanywa na askari maalumu wa usalama barabarani.

Akiwatunuku vyeti vyao, Kiteve alisema madereva wasiziogope sheria za barabarani kwani zina manufaa kwao na kwa watumiaji wengine wa barabara.

Pamoja na kutekeleza sheria hizo, aliwataka madereva kuhakikisha pikipiki wanazoendesha zinalipiwa kodi kama sheria zinavyotaka.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment