Thursday, 3 December 2015

KIMBE WA CHADEMA AWA MEYA MPYA MANISPAA YA IRINGA


DIWANI wa kata ya Isakalilo, Alex Kimbe (Chadema) jana alichaguliwa kwa kura 21 kuwa Meya wa Manispaa ya Iringa.

Kuchaguliwa kwa Kimbe kumemaliza mvutano wa ndani kwa ndani uliokikumba chama hicho wakati kikiwa katika mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi hiyo na kumaliza historia enzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoa Meya kila baada ya Uchaguzi Mkuu.

Katika kinyang’anyiro hicho ambacho CCM walikuwa wasindikizaji kwasababu ya kuwa na idadi ndogo ya madiwani; mgombea wake Bashir Mtove alijipatia kura 6.

Mtove aliwania nafasi hiyo iliyoachwa wazi na aliyekuwa Meya wa miaka mingi wa manispaa hiyo, Amani Mwamwindi ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, alishinda kwa kura chache kiti cha udiwani wa kata ya Mlandege dhidi ya mgombea wa Chadema, Richard Mfune.

Baraza hilo la madiwani lilimchagua pia Joseph Lyata wa Chadema kuwa Naibu Meya kwa kujinyakulia kura 21 dhidi ya kura 6 alizopata Dora Nziku wa CCM.

Awali katika salamu zake kwa madiwani hao, Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi aliwataka madiwani na halmashauri hiyo kufanya kazi, kupunguza tambo za barabarani na kushirikiana na wananchi kuleta maendeleo kupitia Ilani ya CCM.

Chadema imeunda halmashauri hiyo baada ya kufanikiwa kushinda kata 14 kati ya 18 za Jimbo la Iringa Mjini linaloongozwa kwa awamu ya pili na Mchungaji Peter Msigwa aliyemshinda mgombea wa CCM, Frederick Mwakalebela katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Reactions:

1 comments:

  1. kuna watu walisema msigwa akichukua tena udiwani wanahama hapo IRINGA vipi wameshahama?? nisalimieni wote hapo rafiki zangu akina Fransisi, Raymond minja, Clement sanga n.k

    ReplyDelete