Friday, 11 December 2015

KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA ATOA MAAGIZO HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA MBEYA


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donald Mbando, ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa hospitali ya rufaa ya kanda iliyopo mkoani Mbeya kuhakikisha inakamilisha ukarabati wa maabara ya kupimia magonjwa yanayoambukiza haraka ikiwemo Ebora.

Dk Mbando alitoa maagizo hayo jana alipotembelea wizara hiyo kujionea maendeleo ya ukarabati wa maabara, wodi za wagonjwa na ujenzi wa jengo la vipimo vya uchunguzi.

Akizungumza na uongozi wa hospitali hiyo, katibu mkuu alisema ametoa wiki mbili kwa hospitali hiyo kukamilisha ukarabati wa jengo la maabara ili lianze kutumika kwa kazi za upimaji magonjwa hayo na mengine mbalimbali.

Aliuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha ndani ya wiki moja inampelekea  mchanganuo wa fedha za kumalizia ujenzi wa jengo hilo ambalo tayari limetumia Sh Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wake wa awamu ya kwanza.

Alisema kukamilika kwa jengo hilo kutawapunguzia gharama, wateja wake wengi, wanaotakiwa kusafiri hadi Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo hivyo.

Alivitaja vipimo vingine vitakavyowekwa katika jengo hilo kuwa ni pamoja na X- ray, ultra sound na ct scan.

Katibu mkuu pia aliagiza hospitali zote nchini kuanzia za wilaya, mikoa na  za rufaa za mikoa na kanda  kuhakikisha zinakuwa na mfumo wa Elekitroniki kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato ili kupunguza mwanya wa upotevu wa fedha na ubadhilifu.

Alisema mfumo huo pia utasaidia kurahisisha mawasiliano baina ya madaktari kwa madaktari au hospitali moja na nyingine kuhusiana na tatizo la ugonjwa pindi tatizo linapokuwa kubwa.

Aidha aliupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato baada ya kuanzisha mfumo wa TEHAMA, kutoka Sh Milioni 50 kwa mwezi hadi zaidi ya Sh Milioni 500.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment