Friday, 18 December 2015

KAMPENI YA ABIRIA PAZA SAUTI YATOA NAMBA ZA KUDHIBITI AJALI MKOANI IRINGA

KAMATI ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Barabarani imetoa namba za simu kwa abiria wakati wakizindua mkoani hapa, kampeni yao ya Abiria Paza Sauti.

Kampeni hiyo inayolenga kupunguza ajali katika kipindi cha kuelekea siku kuu za Krismasi na Mwaka mpya, ilizinduliwa juzi jioni katika stendi ndogo ya mabasi yaendayo mikoani ya Ipogolo, mjini Iringa.

Mratibu wa Kanda ya Nyanda za Juu wa Mabalozi wa Usalama Barabarani, Ramadhani Msangi alizitaja namba hizo kuwa ni 0658376053 ya Trafiki Iringa na 0758807734 ya Sumatra Iringa.

Alizitaja namba zingine kuwa ni 0682887722 ya Trafiki Makao Makuu Dar es Salaam na 0800110019/20 ya Sumatra Makao Makuu Dar es Salaam.

Msangi alisema kwa kupitia namba hizo, abiria wanatakiwa kupaza sauti zao kama kauli mbiu ya kampeni yenyewe inavyotaka kwa kuwaripo madereva wanaokwenda mwendo kasi, wanaofanya ovateki hatarishi, walevi na wanaokiuka sheria nyingine zote za barabarani.

“Kampeni hii inatwaka pia abiria wakatae kulanguliwa tiketi, kusafiri na dereva mmoja safari ndefu na kupanda gari lisilo na mikanda kwa kutoa taarifa kupitia namba hizo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mara moja,” alisema.

Akizindua kampeni hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Asas alisema; “tunashirikiana na mabalozi wa usalama barabarani kuhakikisha kwamba abiria wanafanya safari zao kuanzia maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa  wanashiriki kuzuia ajali za barabarani.”

Asas aliipongeza kampeni hiyo akisema imekuja katika kipindi mwafaka cha mwezi Desemba ambacho rekodi zake zinaonesha ndicho kipindi kinachokuwa na ajali nyingi za barabarani.

“Kumbukumbu zetu zinaonesha kuwepo kwa matukio mengi ya ajali za barabarni katika kipindi cha mwezi hu wakati wananchi wakizikaribisha siku kuu za krismasi na mwaka mpya,” alisema.

Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Leopord Fungu alisema; “pamoja na kwamba kampeni hii inalenga kipindi hiki cha mwezi Desemba, hapa Iringa tunataka iwe ya kudumu.”

Aliwataka abiria kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi kupitia namba hizo za simu ili kunusuru mali na maisha ya watu wawapo safarini.

Akizungumzia vitendo vya rushwa barabarani, Fungu aliwataka abiria kutumia pia namba hizo kutoa taarifa za askari wote wa usalama barabarani wanajihusisha na vitendo hivyo pamoja na kukiuka maelekezo mengine ya kazi yao wawapo barabarani.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment