Thursday, 24 December 2015

KAIMU MKURUGENZI WA OCEAN ROAD ANG'OLEWA

Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu .

Waziri  wa  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  ametangaza kumsimamisha kazi kazi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Diwani Msemo.

Mkurugenzi huyo amesimamishwa kupisha uchunguzi utakaobaini kama kulikuwepo na mgongano wa kimaslahi ulioathiri utendaji wa taasisi  hiyo chini ya kiongozi huyo.

Tangu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu; katika kampeni zake nchini kote, Rais Dk John Magufuli alikuwa akizungumzia kukosekana kwa dawa katika hospitali za Serikali huku vituo vya afya vya  binafsi vikiwa na dawa.

Pamoja na Rais kuahidi kupambana na suala hilo, taarifa ya waziri huyo inaonesha upungufu wa dawa na vifaa tiba katika hospitali za umma unaendelea kujitokeza huku baadhi ya wagonjwa wakieleza kwa uchungu jinsi wanavyopata dawa kwa tabu zikiwemo zile zinazotakiwa kutolewa bure au kwa bei ya ruzuku.

Wakati akimsimamisha kazi mkurugenzi huyo, Mwalimu ameagiza watendaji wote wa sekta ya afya hususani wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya, Wafamasia, Wauguzi na Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kukiri kwa maandishi kwa ngazi zao za uwajibikaji endapo wanamiliki hospitali, zahanati, kliniki, maduka ya dawa ndani ya siku 21 kuanzia jana desemba 23.

 Lengo la kupata taarifa hiyo linalenga kuziba mianya ya upotevu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya umma.

Kufuatia kusimamishwa  kwa Bw. Msemo  Bodi ya Taasisi ya Ocean Road imeagizwa kutafuta mtu atakayekaimu nafasi iliyoachwa wazi na Dk.Msemo anayefanyiwa uchunguzi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment