Friday, 4 December 2015

JELA MIAKA 25 KWA KUAMBUKIZA WATU 200 VVU

Daktari bandia akiwa chini ya ulinzi

Daktari aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kuwaambukiza wagonjwa 200 Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini Cambodia amehukumiwa jela.

Daktari huyo bandia alipatikana na hatia ya kuwaambukiza takriban watu hao virusi vya ugonjwa wa Ukimwi amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa hilo ambapo limesababisha baadhi ya wagonjwa hao kufariki.

Inadaiwa kuwa Yem Chrin, alikuwa akitumia sindano zilizokuwa zimekwisha tumika kuwatibu wenyeji wa kijiji cha Roka, bila ya kujua alikuwa akisambaza Virusi vya Ukimwi.

Awali Chrin, alikuwa ameshtakiwa kwa mauaji lakini upande wa mashtaka ukabadilisha shtaka na kuwa shtaka la kuua bila ya kukusudia.

Sambamba na hilo inadaiwa kuwa kesi hiyo imefichua uhaba wa madaktari na ugumu uliopo kwa raia kupata huduma za afya katika maeneo mengi ya vijijini nchini Cambodia.

Utafiti umebaini kuwa zahanati nyingi katika maeneo ya vijijini huendeshwa na madakatari bandia ambao hawajahitimu mafunzo ya kuwatibu wagonjwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment