Thursday, 17 December 2015

DK MAGUFULI ALIVYOMNG'OA HOSEAH TAKUKURU NA KUWASIMAMISHA KAZI WALIOKAIDI AGIZO LA KUTOSAFIRI NJE YA NCHI


RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk Edward Hoseah. Aidha, ameamuru kusimamishwa kazi kwa watumishi waandamizi wanne wa taasisi hiyo kwa kukiuka maagizo yake.

Rais ametengua uteuzi huo wa Dk Hoseah, kutokana na kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa, hususan kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam jana kwa niaba ya Rais, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alisema kutokana na kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.

Balozi Sefue alibainisha kuwa Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa Takukuru chini ya Dk Hoseah, hauwezi kuendana na kasi anayoitaka.

“Eneo mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya serikali ni bandarini na katika Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, hivyo Mheshimiwa Rais amesikitishwa na kitendo cha taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika eneo hilo kwa muda mrefu, lakini kasi ya Takukuru kuchukua hatua haiendani na kasi anayoitaka,” alisisitiza Balozi Sefue.

Dk Hoseah alichaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru mwaka 2006, na hivyo amedumu katika wadhifa huo kwa takribani miaka tisa sasa. Alitanguliwa na Meja Jenerali mstaafu, Anatory Kamazima ambaye aliiongoza Takukuru kuanzia mwaka 1990 hadi 2006.

Wakurugenzi wengine waliowahi kuiongoza Takukuru ambayo awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) ni Geofrey Sawaya (1973 – 1974), S. Rutayangirwa (1974 – 1975) na Zakaria Maftah (1975 – 1990).

Kwa mujibu wa sheria, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru huteuliwa na Rais, na anasaidiwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu, wadhifa alionao Mlowola ambaye kabla ya uteuzi huo uliofanywa Oktoba 23, mwaka huu, alikuwa Mkurugenzi wa Intelijensia ya Makosa ya Jinai katika Jeshi la Polisi nchini.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Takukuru waliosafiri nje ya nchi, licha ya Rais kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.

Watumishi hao ni Mkurugenzi Elimu kwa Umma, Mary Mosha, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Ekwabi Mujungu, Mkurugenzi wa Uhusiano, Doreen Kapwani na Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi Mkuu, Rukia Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.

Kutokana na hatua hiyo ya Rais Magufuli, Balozi Sefue amewataka watumishi wengine wa umma, kutii agizo la Rais na kuonya kuwa atakayekiuka atachukuliwa hatua kali. Katika moja ya hatua za kubana matumizi ya serikali, Rais Magufuli alitangaza kufuta safari zote za nje kwa watumishi wa umma, isipokuwa kwa vibali maalumu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment