Thursday, 24 December 2015

DK MAGUFULI AKAMILISHA UTEUZI BARAZA LA MAWAZIRI


Rais John Magufuli amemalizia kujaza nafasi za uteuzi wa mawaziri na naibu waziri alizobakiza wakati akitangaza Baraza la Mawaziri la kwanza la Serikali ya Awamu ya Tano.

Katika taarifa iliyotolewa jana usiku na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, walioteuliwa ni Profesa Jumanne Maghembe ambaye anakuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Philip Mpango kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Gerson Lwenge kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Dk Joyce Ndalichako kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.

Katika uteuzi huo, Rais Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya Baraza hilo kwa kumhamisha Profesa Makame Mbarawa kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwenda Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Pia, amemteua Hamad Masauni kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mawaziri wapya
 Kabla ya uteuzi huo, Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, alikuwa Waziri wa Maji katika Serikali iliyopita akiwa pia amewahi kuongoza wizara hiyo ya maliasili. Nyingine alizowahi kuongoza ni Kazi na Ajira na Elimu.

Mhandisi Lwenge ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Magharibi, alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi akifanya kazi chini ya Dk Magufuli katika Serikali iliyopita.

 Dk Mpango ambaye pia ameteuliwa kuwa mbunge, hivi karibuni aliteuliwa na Dk Magufuli kuwa kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kumsimamisha kazi, Rished Bade kutokana na kashfa ya upotevu wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kama ilivyokuwa kwa Dk Mpango, Dk Ndalichako ambaye pia ameteuliwa kuwa mbunge aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Akizungumzia uteuzi huo, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR­Mageuzi, James Mbatia alisema kitendo cha Rais Magufuli kumhamishia wizara nyingine Profesa Mbarawa kunadhihirisha jinsi alivyokosa utulivu katika uteuzi. Alisema ili nchi iweze kusonga mbele, inahitaji iwe na mfumo imara wa utawala ambao hauwezi kupatikana kama nchi haitakuwa na Katiba Mpya, kanuni na taratibu nzuri.

“Mawaziri wameteuliwa Desemba 10 na kuapishwa siku mbili baadaye. Leo (jana) ni siku ya 13 tangu wateuliwe tayari waziri mmoja amehamishwa wizara.”

 “Dk Magufuli akitaka kuongoza nchi arudi katika msingi wa kubadili mfumo. Kasi ya mabadiliko ya dunia hatuwezi kwenda nayo sambamba kama tutaendelea kuwa na mfumo mbovu,” alisema Mbatia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment