Tuesday, 29 December 2015

DC ATOA SIKU 21 KWA WALIOWEKEZA KARIBU NA VYANZO VYA MAJI NA HIFADHI YA BARABARA WAONDOKE


AKIENDANA na matakwa ya serikali ya awamu ya tano,Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera ametoa siku 21 kwa watu wote waliojenga nyumba katika hifadhi au maeneo ya barabara na karibu na vyanzo vya maji, kubomoa kabla kazi hiyo haijafanywa na mamlaka zinazohusika.

Kasesera alitoa agizo hilo Desemba 24 alipokuwa akijibu risala ya wananchi wa kijiji cha Igwachanja kilichopo nje kidogo ya manispaa ya Iringa walioomba wadau wawasaidie kujenga zahanati na kituo cha Polisi, kijijini hapo.

Risala hiyo ilisomwa na Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Charles Matunduru wakati mkuu wa mkoa wa Iringa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kutibu nguzo za umeme na bidhaa zingine zitokanazo na miti, kinachojengwa na kampuni ya Agora Wood Products Ltd.

“Kwa kupitia hadhara hii, niwatangazie wale wote waliojenga nyumba katika meneo yasioruhusiwa kisheria, iwe ndani ya barabara au katika maeneo mengine yasiyoruhusiwa; au wale wanaolima au kufanya shughuli mbalimbali kama vile uchomaji wa tofali karibu na mito, natoa siku 21 wawe wameondoka,” alisema.

Alisema baada ya siku hizo 21 kupitia serikali itatumia rasilimali zake kubomoa maeneo hayo na wanaohusika watapaswa kufidia gharama zake.

“Kwa wale walioko karibu na mito wajue sheria inataka wafanye shughuli zao mita 60 kutoka katika kingo za mito, kwahiyo natoa wito kwao waanze kuondoa vitu au mali zao zilizopo ndani ya mita hizo,” alisema.

Alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa sheria zote ikiwemo sheria ya mazingira ili kuyalinda mazingira hayo kwa ajili ya  vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Ukiugua lazima sindano ichomwe panapohusika, iingie vizuri ili mgonjwa apone; ambianeni wote mliojenga barabarani, maeneo yasiyoruhusiwa au yenye matatizo kisheria, wachoma tofali, wakulima na wengineo, kwamba bomoeni au ondokeni kabla sindano haijawafikia,” alisema.

Akijibu maombi ya wananchi wa kijiji hicho, Kasesera alivitaka vijiji kupunguza ombaomba kwa wawekezaji akisema tabia hiyo wakati fulani inapunguza mahusiano na wawekezaji hao.

“Tutumie nguvu kazi tuliyonayo kujenga miradi ya maendeleo katika vijiji vyetu. Ujenzi wa zahanati na kituo cha polisi unahitaji kwanza nguvu za wananchi wenyewe kabla wadau wetu wa maendeleo hawajaombwa kuchangia,” alisema.

Akiipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji inayofanya kijijini hapo, mkuu wa wilaya alisema uwekezaji una faida kubwa kwa kizazi cha sasa, baadaye na maendeleo ya Taifa.

Alisema vijana wengi wanaweza kubadili maisha yao na ya familia zao kama wanachokipata hawatakipeleka kwenye anasa kama wafanyavyo vijana wengi.

“Asilimia kubwa ya  vijana, fedha zao zinaishia kuhonga, kunywea pombe, kwenye starehe za muziki, wasapu na anasa zingine,” alisema wakati akiwasifia vijana tisa walioanzisha kampuni hiyo inayojenga kiwanda hicho kijijini hapo.

Kampuni hiyo ya Agora Wood Products Ltd inamilikia na vijana tisa wa kitanzania ambao wamechangishana zaidi ya Sh Milioni 500 na kuanza ujenzi wa kiwanda hicho cha kutibu nguzo katika kijiji hicho.

Afisa Mtendaji wa kampuni hiyo, Elisha Msengi alisema wameanzisha kampuni hiyo kwa lengo la kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika sekta ya misitu ili kuzalisha bidhaa zitokanazo na misitu zenye ubora wa kiwango cha juu na kuziuza ndani na nje ya nchi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment