Wednesday, 9 December 2015

BENKI MBILI ZAVAMIWA, ASKARI WALINZI WAUAWA, WATU WAJERUHIWA WAPORWA


WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi wanaokadiriwa kuwa sita, leo wamevamia benki za DCB na CRDB na kuua askari wawili wa SUMA JKT kisha kupora fedha ambazo hazijajulikana ni kiasi gani.  

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya alisema tukio hilo lilitokea alasiri eneo la Chanika Mwisho, ambako watu hao waliokuwa katika pikipiki kati ya tatu au nne walivamia benki hizo.  

Kamanda Mkondya alisema watu hao wanaodhaniwa kuwa majambazi walikuwa wamepakiana katika pikipiki hizo waliwaua askari hao na kujeruhi watu wengine wanne waliokimbizwa hospitali kwa matibabu.  

Alisema benki hizo mbili zimeanzishwa hivi karibuni katika maeneo hayo, hivyo walitumia fursa hiyo kufanya uhalifu huo.  

“Ni kweli hili tukio limetokea, lakini mpaka sasa bado haijajulikana ni fedha kiasi gani kimeporwa, pengine ukinipigia baadaye naweza kukupa kiwango cha fedha kilichoporwa kama nitakuwa nimepata,” alisema Kamanda Mkondya.  

Alisema watu hao si majambazi wa kawaida kutokana na uzoefu wa matukio ya uvamizi wa vituo na Benki ya NMB Mkuranga.  

Kamanda Mkondya alisema majambazi hao baada ya kufanya tukio hilo walikimbilia upande wa kusini ambao kuna mapori.  

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu hao na kuhakikisha linawakamata na kuwafikikisha mahali kunakostahili ili sheria ichukue mkondo wake.
Source:Habarileo  

Reactions:

0 comments:

Post a Comment