Friday, 18 December 2015

BASI LA NEW FORCE LAPATA AJALI IRINGA, 12 WAFARIKI DUNIA, 28 WAJERUHIWA



ABIRIA 12 wamefariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa, wengine vibaya, baada ya basi walilopanda, mali ya kampuni ya New Force lililokuwa likitokea Dar es Salaam kulekea Tunduma Mbeya kugongana na roli lililokuwa likitokea Mafinga mkoani Iringa likielekea Dar es Salaam.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Peter Kakamba amethibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ajali hiyo imetokea majira ya 7.30 mchana katika eneo la Igeme
kata ya Mahenge wilayani  Kilolo mkoani Iringa.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya lori hilo lenye namba za usajili T 616 BEF aina ya Scania lilokuwa na tela namba T 320 BEF kupasuka tairi la mbele na hatimaye kulivaa basi hilo lenye namba T483 CTF.

Alisema majina ya watu waliofariki ambao kati yao wanaume wako nane na wanawake wanne hayakuweza kupatikana mara moja na kwamba utambuzi unaendelea.

Aliwataja majeruhi waliokimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Iringa kuwa ni pamoja na Michael Mahenge (40), Hawadi Msigwa (27) na Eliud Kalinga (20) wote wakazi wa Tunduma, Nicholaus Charles (45) mkazi wa DSM,  Lulu Norbeth (15) na AntonMwashiuya (43) waazi wa Mbozi, Mbeya.

Wengine ni  Juma Wiliam Lucas Wilian, Willson Ndumba, Anitha Obadia Sanga, Arapha Hamdan, Razak Ngai na James Duma (49) raia wa Afrika Kusini.

Majeruhi wengi ni Jonas, Kasungu Kabanga raia wa Congo, Frank Kalinga, Silverster Ndenye, Aizack Ndula, Lulu Ndula na Suma Japhet.

Naye Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa  , Dk useleta Nyakiroto amethibitisha kupokea kwa miili ya marehemu na majeruhi.

“Kweli nimepokea miili ya marehemu 12 na tunaendelea  kufanya utambuzi na ajeruhi 28 ambao pia tunaendelea na utambuzi wao .”alisema Nyakiroto.

 Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo na majeruhi wanaendelea na matibabu na hali zao zitapoonekana kuimarika wataruhusiwa. 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment