Monday, 14 December 2015

BASHE AMKATAA MGANGA MKUU WA WILAYA YA NZEGA


MBUNGE wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe amemkataa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Emmanuel Mihayo kwa madai ya kushindwa kusimamia na kutatua matatizo mbalimbali ya watumishi wa afya, hali inayosababisha hospitali hiyo kugubikwa na migogoro dhidi ya watumishi wake.

Bashe akiwa katika ziara ya kikazi hospitalini hapo na kubaini matatizo mbalimbali yanayowakabili watumishi na wagonjwa, alisema mganga huyo ameshindwa kuwajibika ipasavyo kwa watumishi ikiwamo kutatua kero zao.

Alisema watumishi hao wanakabiliwa na matatizo ya mishahara, kutolipwa fedha za muda wa ziada, kutopewa fedha za sare za kazi na mapunjo, hali inayowafanya washindwe kuwajibika ipasavyo kwa wateja wao.

Alipoulizwa sababu nyingine ya kumkataa mganga huyo ambaye kwa sasa yupo likizo ya masomo katika Hospitali ya Rufaa Bugando, alisema ni kugawa fedha za matumizi ya ziada kwa watumishi akiwa chuoni na kukusanya fedha za tozo za baiskeli Sh 200 kwa wagonjwa wanaoingia katika hospitali hiyo kwa ajili ya ulinzi na mali zao.

Alisema mganga huyo amekuwa akisikia fedha za matumizi ya ziada zimefika katika hospitali hiyo amekuwa akiacha masomo na kwenda kugawa fedha hizo kwa watumishi wakati akihesabika yupo likizo na kuongeza kuwa hali hiyo inatia shaka kiutendaji wa kazi kwa mtumishi huyo.

 “Siwezi kuvumilia hii hali, huyu simtaki hata kidogo ameshindwa kutekeleza wajibu wake hatuwezi kuwa na mtu kama huyo yupo likizo ya masomo, lakini akisikia pesa imekuja ya matumizi ya ziada anakuja kugawa pesa yeye kama nani simtaki hapa ananiletea migogoro,” alisema Bashe.

 Mganga wa zamu, Amos Peter akijibu maswali na kumuongoza mbunge huyo, alisema malalamiko hayo yamekuwa na muda mrefu kwa uongozi na hakuna jitihada zilizochukuliwa za kuwasaidia watumishi hao.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya, Emmanuel Mihayo alipopigiwa simu yake ya mkononi, alisikitishwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na mbunge na kuongeza kuwa hana kosa lolote katika hospitali hiyo na kwamba matatizo ya watumishi ni ya muda mrefu ambayo yanapaswa kutatuliwa na Halmashauri ya Wilaya.


“Nimeshangazwa sana kuambiwa hivyo. Hakuna ukweli wowote na hayo madai ni yamuda mrefu na mimi nimeyakuta hapo na taarifa mbalimbali zipo ofisi ya mkurugenzi, mimi sihusiki kabisa katika hilo,” alisema Mihayo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment