Tuesday, 22 December 2015

AS SALAAM YAZINDUA HUDUMA YA USAFIRI WA ANGA IRINGA DAR KWA BEI NAFUU


KAMPUNI ya As Salaam Air imesikia na kukifanyia kazi kilio cha ongezeko la abiria wa usafiri wa anga mkoani Iringa baada ya kuanzisha huduma ya safari ya Dar es Salaam, Iringa, Dar es Salaam itakayotolewa mara tatu kwa wiki.

Usafiri huo wa ndege utakaokuwepo kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ulianza kutolewa juzi, katika hafla iliyozinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera katika uwanja wa ndege wa Nduli, mjini Iringa.

Ilikuwa majira ya saa 6.30 mchana, ndege ya kampuni hiyo ilipowasili katika uwanja huo na ikamwagiwa maji na gari la zimamoto la Manispaa ya Iringa wakati ikipita kuelekea eneo la maegesho kama ishara ya kupokea huduma yake.

Mkuu wa wilaya ya Iringa alipanda na kushuka katika ndege hiyo baada ya abiria waliokuwemo, wakitokea Dar es Salaam kushuka na wale waliokuwa wakisafiri kuelekea Dar es Salaam kuingia kwa ajili ya safari yao.

Akizindua huduma hiyo, Kasesera aliipongeza kampuni inayomiliki ndege hiyo kwamba wameleta huduma “kwa watu wenye fedha mkoani Iringa.”

“Niwaombe wana Iringa tujifunze kujali muda. Sio mara zote tunatakiwa kusafiri kwa njia ya barabara kwasababu huduma hiyo inatumia muda mrefu na inachosha pamoja na uzuri wake, sasa tumeletewa ndege, cha msingi ni kuomba gharama zake ziwe zinazozingatia mahitaji ya soko kwasasa,” alisema.

Alisema wakati serikali ikiwa katika mpango wa kupanua uwanja huo wa ndege ili kuziwezesha ndege kubwa zaidi kutua, kuna haja ya uwanja huo kuwa na sehemu kubwa ya maegesho ya ndege ili safari zingine za ndege ziwe zinaanzia katika uwanja huo.

Rubani wa ndege hiyo Ismail Haji Nuru alisema kampuni hiyo ilianza kutoa huduma za anga miaka minne iliyopita, ikifanya safari za Dar es Salaam, Zanzibar, Pemba na Tanga.

Alisema katika kuboresha huduma hiyo wameamua kutanua huduma hiyo kwa kuanzisha safari ya Iringa, Songea na Dodoma na Januari 15 watakuwa na ndege kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 30.

“Kuja kwa ndege hiyo kutapunguza zaidi gharama za usafiri na muda wa safari angani,” alisema huku akiahidi kwa niaba ya kampuni hiyo, kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo mkoani Iringa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment