Monday, 9 November 2015

TEMBO WA RUAHA WAFUNGWA KIFAA CHA MAWASILIANO KITAKACHOSAIDIA KUWANASA MAJANGILI


ULINZI na usalama wa Tembo wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha umeongezeka baada wanyamapori hao wanaowindwa na majangili wa meno yake kufungwa kifaa maalumu (Kola) kinachofuatilia mienendo yao ya ndani na nje ya mfumo wa Ikolojia ya Ruaha.

Ufungaji wa Kola kwa wanyamapori hao wanaoliingiza Taifa fedha nyingi za kigeni kwa njia ya utalii; umefanywa na Taasisi ya World Elephant Centre (WEC) kupitia Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mtafiti Mwandamizi wa WEC, Dk Alfred Kikoti alisema Kola inatumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya setilaiti ya utambuzi wa jiografia ya maeneo (GPS) na kompyuta.

Kwa kupitia teknolojia hiyo Dk Kikoti alisema mienendo ya wanyama hayo itakuwa ikiripotiwa kwenye setilaiti na kurushwa moja kwa moja katika chumba maalumu cha ulinzi.

“Kwahiyo teknolojia hii itatuwezesha kujua mwenendo wa tembo ndani na nje ya hifadhi; tutajua walipo, wanapopita, kasi yao ya kutembea, sehemu wanazojificha, wanazokunywa maji, wanazopumzika, maeneo wanayokaa kwa muda mrefu, kama wamekufa, wamejeruhiwa, wamehama hifadhi moja hadi nyingie na taarifa nyingine nyingi hivyo itakuwa rahisi kwa askari wa wanyamapori kufuatilia usalama wao,” alisema.

Dk Kikoti alisema kwa kuzingatia kwamba Tembo wana kawaida ya kutembea katika makundi makubwa, Kola hizo zenye uwezo wa kufanya kazi kwa miaka mitatu bila kubadili betri zake zinafungwa kwa Tembo 30 wanaoongoza makundi 30.

Alisema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo linalogharimu Dola 15,000 (Sawa na Sh Milioni 30) kwa Tembo mmoja, askari wa doria wataweza kufanya doria kwa kuongozwa na taarifa zitakazotolewa na kola tofauti na sasa ambapo hufanya kwa kukisia tu.

“Zoezi la ufungaji kola kwa tembo mmoja huchukua wastani wa dakika 30, likihusisha matumizi ya helkopta kwa ajili ya kubaini yalipo makundi ya Tembo na uchomaji wa sindano ya usingizi kwa Tembo anayefungwa Kola, ufungaji wa Kola na uchomaji wa sindano ya kumzindua,” alisema.

Akizungumzia mafanikio ya mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi alisema eneo la mfumo wa ikolojia ya Ruaha ni kubwa na lina tembo wengi kuliko eneo jingine Tanzania hivyo haina budi kuangaliwa kwa ukaribu zaidi.

“Tunafurahi kwamba Kola hizo zitaunganishwa na mifumo ya mawasiliano na kuliwezesha shirika kufanya kazi ya ulinzi kwa ufanisi zaidi kwa kuhakikisha kila wanapokuwepo wanyama hao, askari wanakuwepo pia,” alisema na kuongeza kwamba mpango wa ufungaji wa kola kwa Tembo utafanywa pia katika hifadhi zingine zote.

Naye Mratibu wa SPANEST, Godwel Ole Meing’ataki alisema zoezi la ufungaji wa kola kwa tembo ni moja ya shughuli ya mradi huo katika harakati za kuwalinda tembo na kupambana na ujangili.

Alisema kwa kupitia kifaa hicho askari wa wanyamapori watakabiliana kirahisi na majangili wa meno ya tembo katika azma ile ile ya kunusuru kiumbe hicho kinacholiingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.

Pamoja na Tembo hao kufungwa kifaa hicho, Meing’ataki alisema wadau wa uhifadhi hawana budi kuendelea na mikakati mingine ya kukabiliana na ujangili ili kwa pamoja mipango hiyo imalize kabisa tatizo hilo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment