Tuesday, 17 November 2015

NI JOB NDUGAI SPIKA WA BUNGE LA 11


Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (CCM), ndiye Spika wa Bunge la 11 baada ya kuchaguliwa kwa jumla ya 254 kati ya kura 365 zilizopigwa ndani ya Bunge leo .

Ndugai amewashinda wagombea wengine saba.

Ndugai aliyekuwa Naibu Spika  katika Bunge la Kumi lililomalizika Agosti 21, mwaka huu, alitwaa nafasi hiyo baada ya kupata asilimia 70  ya kura zote zilizopigwa.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Bunge, ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Dk. Thomas Kashililah, alisema Ndugai alipata kura 254 akifuatiwa na mgombe wa Chadema, Godluck Ole Medeye aliyepata kura 109.

Wagombea wengine sita na vyama vyao katika mabano hawakupata kura, ambao ni Peter  Leonard Sarungi (AFP), Hassan  Kisabya Almas (NRA), Dk. Godfrey Fatael Malisa (CCK), Richard Shedrack Lyimo (TLP), Hashim Spunda Rungwe (Chauma) na Robert Alexander Kasinini (DP).

Mwenyekiti  wa kikao cha uchaguzi, alikuwa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.

Chenge aliteuliwa kuongoza kikao hicho kutokana na kuwa Mbunge aliyekaa muda mrefu zaidi, ambapo amekuwa bungeni tangu mwaka 1993 alipoteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo Rais akiwa Ali Hassan Mwinyi, kisha akateuliwa tena mwaka 1995 katika nafasi hiyo hiyo wakati Rais akiwa Benjamin Mkapa, kabla ya mwaka 2005 kugombea ubunge Bariadi nMagharibu nafasi anayoishikilia hadi sasa.

Kutokana na ushindi huo, Ndugai anakuwa Spika wa sita wa bunge hilo, ambapo wengine ni hayati Adam Sapi Mkwawa kuanzia 1964 hadi Novemba 19, 1973, kisha akaingia Erasto Mang'enya Novemba 20, 1973 hadi Novemba 5, 1975, kisha akarudi tena Mkwawa kuanzia Novemba 6, 1975 hadi Aprili 25, 1994.


Wengine ni Pius Msekwa Aprili 28, 1994 hadi Novemba 20, 2005, Samuel Sitta Desemba 26, 2005 hadi Novemba 2010, kisha Makinda Novemba 12 hadi jana.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment