Tuesday, 10 November 2015

NABII WA IRINGA AJA NA UJUMBE WA MUNGU UNAOMTAKA DK MAGUFULI KUUNDA SERIKALI YA MSETONABII Israel Hekima ya Moto wa mjini Iringa amemtaka Rais wa awamu ya tano, Dk John Pombe Magufuli kuunda serikali ya mseto itakayoshirikisha viongozi na wabunge kutoka kambi ya upinzani.

Akizungumza na wanahabari katika ofisi ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC) jana, Nabii huyo aliyeko mbioni kuanzisha kanisa lake baada ya kuacha kuabudu katika kanisa la Siloam la mjini alisema:

“Katika maono niliyopewa na Mwenyezi Mungu baada ya shughuli ya kuchagua viongozi wetu kukamilika kuna ujumbe kwa Rais wetu mpya unaotaka serikali ya Dk Magufuli inayotakiwa kuhusisha viongozi kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa kufanya kazi kwa kuzingatia amri za Mungu.

Nabii Israel alisema Rais anatakiwa kuwa na angalizo katika uteuzi wa watu wanaoweza kumsaidia kuendesha serikali kwa misingi ya kweli na haki na ili aweze kufanikiwa ni lazima apate baadhi yao kutoka nje ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Mungu anasema katika maono aliyonipa kwamba Dk Magufuli anajua kwamba kuna watu wengi wazuri nje ya chama chake wanaoweza kumsaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi,” alisema.

Akionesha bahasha aliyodai ndani yake ina maelekezo hayo na mengine muhimu yanayotakiwa kumfikia Rais Dk Magufuli, Nabii Israel alisema anaendelea na jitihada za kukutana na kiongozi huyo wa nchi ili amkabidhi bahasha yenye ujumbe huo.

“Nimeomba kukutana na Rais kwa kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambayo naamini ndiyo inayofanya kazi kwa niaba ya kiongozi huyo,” alisema.

Pamoja na maelezo hayo, Nabii huyo alisema Mwenyezi Mungu amemuagiza ampelekee ujumbe wa kipekee aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwavuli wa vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu aliyejiuzuru, Edward Lowassa.

“Kwa kupitia maono hayo nimeambiwa Lowassa anatakiwa kuachana na siasa na badala yake aanze kuifanya kazi ya kumtumikia Mungu kwani huko ndiko anakohitajika zaidi,” alisema bila kufafanua zaidi.

Alisema jitihada za kumpata Lowassa mwenyewe kwa kupitia simu yake ya mkononi ili amueleze ujumbe huo zimekuwa zikigonga mwamba kwani simu yake imekuwa haipokelewi na kiongozi huyo.

Kuhusu hali ya kisiasa inayoendelea huko Zanzibar, Nabii Israel alisema; “Mungu ameniambia kwamba mshindi katika uchaguzi ule ni Maalim Seif Sharrif Hamad. Kwahiyo tume inatakiwa imtangaze ili aweze kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment