Monday, 2 November 2015

MBUNGE MTEULE MAFINGA MJINI AANZA KWA KUWAKUMBUKA WANAFUNZI WALEMAVU WA SHULE YA MSINGI MAKALALA

MBUNGE Mteule wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi ameanza kuikumbuka jamii anayoiongoza kwa kutoa fedha taslimu na bidhaa mbalimbali kwa wanafunzi walemavu wanaosoma shule ya msingi mchanganyiko Makalala ya mjini Mafinga.

Bidhaa hizo ni pamoja na mafuta kwa ajili ya albino, na miwani, dawa za meno, sukari, sabuni, shampoo, fagio, pipi, mikate, biskuti na Sh 100,000 zitakazotumika kununua nguo za ndani za watoto 23 walemavu wanaosoma shuleni hapo.

Akikabidhi bidhaa hizo kwa wanafunzi hao, Chumi alisema; “badala ya kuchinja mbuzi na kula na timu yangu ya kama wanavyofanya wengine katika kusheherekea ushindi wao, mie nimeingia kazini, tuwakumbuka watoto hao na tukaamua kuchangishana na kununua vitu hivi vichache kwa ajili yao.”

Chumi alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo jipya mkoani Iringa kwa kupata kura 18,379 dhidi ya kura 12,834 alizopata mshindani wake wa jirani, William Mungai wa Chadema na kura 208 za mgombea wa ACT Wazalendo, Mwangiri Mwangiri.

“Nimeanza kwa kuwakumbuka watoto hawa walemavu wa shule hii, nitaendelea kufanya hivyo kwao na kwa wengine kila ninapopata fursa ya kuchangia mahitaji yao. Kazi hiyo itakwenda sambamba na kusimamia utekelezaji wa Ilani yetu ya CCM ili zile ahadi zetu zote tulizoahidi wakati wa kampeni zitekelezwe,” alisema.

Chumi alisema jimbo la Mafinga Mjini lina fursa nyingi za kiuchumi ambazo kama zitatumika vizuri zitasaidia kupunguza changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazowakabili watu wa jimbo hilo.

Kwa upande wake aliyekuwa kampeni meneja wa mbunge huyo mteule, Albert Chalamila aliutaka uongozi wa shule hiyo kwa kushirikiana na timu Chumi, kuandika andiko la mradi na kuliuza kwa wafadhili ili wasaidie maendeleo ya wanafunzi walemavu wanaosoma shuleni hapo.

Akishukuru kwa msaada huo, Mkuu wa shule hiyo, Shem Muheni alisema; "msaada huu unawaongezea faraja wanafunzi hawa kama mnavyowaona wamefurahishwa na hivi vyote mlivyowaletea na kila mmoja anataka apate."

Alisema wanafunzi hao wanaotoka katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe, Iringa na Morogoro wanahitaji misaada wa hali na mali kutoka katika makundi mbalimbali ya jamii ili kukamilisha pale panaposhindwa kukamilishwa na serikali kwa wakati muafaka.

“Watoto hawa wana mahitaji mengi, na baadhi yake ni ya gharama kubwa, kwahiyo ni jambo la kheri pale wadau mbalimbali wa maendeleo wanapojitokeza na kuwasaidia ili nao waweze kukamilisha ndoto zao za kupata elimu wanayoihitaji,” alisema na kumshukuru Chumi kwa msaada huo.

Muheni alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 ilianza kwa kupokea wanafunzi wasioona mwaka 1974 kabla ya kuanza kuchukua watoto wenye mtindio wa ubongo na walemavu wengine miaka iliyofuata.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment