Monday, 2 November 2015

CHUO CHA BIASHARA IRINGA RETCO CHAFANYA MAHAFALI YA PILI, KUANZISHA KAMPASI YAKE DAR ES SALAAM


KIKIWA katika mikakati ya kuwa chuo kikuu, Chuo cha Biashara cha Iringa Retco (IREBUCO) cha mjini Iringa mkoani Iringa, kiko mbioni kufungua kampusi yake jijini Dar es Salaam sambamba na uanzishaji wa kozi nyingine ili kukidhi mahitaji ya soko.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa chuo hicho, Lucas Mwakabungu kwenye mahafali ya pili ya chuo hicho yaliyofanyika juzi chuoni hapo.

Jumla ya wanafunzi 191 walitunukiwa vyeti vyao katika Astashahada na Stashahada katika uongozi na biashara na mafunzo ya Astashahada katika mawasiliano, Tehama na uhasibu.

Akizungumzia historia ya chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 2009, Mwakabungu alisema kati ya mwaka 2010 hadi 2014 chuo hicho kimeweza kutoa wahitimu 596 wa fani hizo.

“Wahitimu wote hao wamekuwa wakijiunga na vyuo vikuu mbalimbali nchini na wengine wameanzisha biashara zao na kujiajiri na wengine wameajiriwa katika sekta binafsi na ya umma zikiwemo serikali za mitaa,” alisema.

Akipongeza mafanikio ya chuo hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayoub alisema; “chuo hiki kimesaidia serikali kutatua tatizo la ajira kwa watanzania, kinatoa elimu kwa vitendo na hivyo kuondoa tatizo la ujinga na umasikini kwa watanzania na kuandaa wajasiriamali ambao watatengeza ajira nyingi zaidi,” alisema.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringaa, Nuhu Mwasumilwe, Ayoub aliwataka wahitimu wawe waadilifu na wazalendo kwa nchi yao, wafanye kazi kwa bidii na kwa wale watakaopata nafasi ya kuendelea na vyuo vikuu wasome kwa bidii ili wafikie malengo waliyojiwekea.

Katika risala yao iliyosomwa na Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Richard Mbilo wahitimu hao walitaja changamoto zinazowakabili wanafunzi wa chuo hicho kuwa ni pamoja na mikopo ya wanafunzi kuwabagua wale wa elimu ya kati, baadhi ya waajiri kukataa kuwapokea kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na baadhi yao kukosa umakini wakati wakijifunza.

“Pamoja na changamoto hizo, kuna ongezeko la ufaulu kwasababu ya mazingira mazuri ya kusomea zikiwemo kompyuta na maktaba ya kisasa,” alisema huku Katibu Tawala huyo akiahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo.

Wahitimu hao waliiomba serikali itoe udhamini kwa wanafunzi wanaokatiza masomo kwasababu ya kukosa ada.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment