Monday, 9 November 2015

10 WAJITOSA KUMRITHI FILIKUNJOMBE LUDEWA, YUPO PIA MDOGO WAKE NA MASANJA MKANDAMIZAJI


MAKADA 10 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwemo mdogo wake wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa miaka mitano iliyopita Deo Filikunjombe, Phillip Filikunjombe wamejitokeza kuwania ubunge wa jimbo hilo.

Uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo uliahirishwa baada ya aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo, Deo Filikunjombe kufariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Oktoba 15, siku 10 kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu.

Mbali na Filikunjombe, wengine waliokufa katika ajali hiyo ni rubani wa helikopta hiyo, William Slaa, Blanka Haule na Egdi Nkwela.

Akizungumza kwa njia ya simu na HabariLeo jana, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo ya Ludewa, Luciano Mbosa aliwataja wana CCM wengine waliojitokeza kuwania ubunge wa jimbo hilo kupitia chama hicho kuwa ni pamoja na msanii wa vichekesho na muimbaji wa nyimbo za injili, Emmanuel Mgaya maarufu kwa jina la ‘Masanja Mkandamizaji’.

Aliwataja wengine kuwa ni Johnson Mgimba, James Mgaya, Zephania Jwahula, Deo Ngalawa, Dk Evaristo Mtitu na Simon Ngatunga.

Alisema wanachama hao wamechukua fomu wakisubiri mkutano mkuu wa chama utakaowapigia kura za maoni kesho Jumanne ili apatikane  mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa jimbo hilo.

Phillip Filikunjombe ni mwanasheria mwandamizi wa Mamlaka ya ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) toka mwaka 2012 mpaka sasa.

Mbali na kufundisha sheria katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kati ya mwaka kati ya mwaka 2010 na2012 amewahi kufanya kazi ya ukufunzi katika chuo kikuu cha Iringa kati ya mwaka 2007 na 2010.

Phillip Filikunjombe ni msomi mwenye Shahada ya uzamili katika sharia (LLM) ya Chuo kikuu cha Stratchclyde cha Uingereza.

Mbali na shughuli zake zinazotokana na taaluma yake hiyo, mgombea huyo ni Mkurugenzi na mmiliki wa Kampuni ya uwakili ya Reliance Legal Consultants ya Dar es Salaam anayemiliki pia kampuni ya usafiri ya Matatu Logistics.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment