Thursday, 8 October 2015

WANAHABARI IRINGA KUWAKUTANISHA KATIKA MDAHALO WAGOMBEA UBUNGE IRINGA MJINI


KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC) itawakutanisha wagombea ubunge sita wa Jimbo la Iringa Mjini katika mdahalo utakaofanyika ndani ya ukumbi wa Highlands mjini Iringa.

Mdahalo huo utakaofanyika Oktoba 11 kuanzia saa 6.00 mchana hadi saa 10 jioni unalenga kuwawezesha wagombea hao kunadi sera za vyama vyao na mikakati waliyonayo katika kuwalatea wananchi wa jimbo hilo maendeleo.

Wagombea hao ni pamoja na Frederick Mwakalebela (CCM), Mchungaji Peter Msigwa (Chadema na Ukawa), Chiku Abwao ACT Wazalendo, Daudi Masasi (ADC), Robert Kisinini (DP) na mgombea wa Chausta.

Mwenyekiti wa IPC, Frank Leonard alisema mdahalo huo unakuwa wa kwanza katika mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka huu kuwakutanisha wagombea kutoka vyama Vyote vinavyowania nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Mchungaji Msigwa, miaka mitano iliyopita.

Kwa kupitia mdahalo huo Leonard alisema, wagombea hao ambao wote wamethibitisha kushiriki wanatarajia kurudisha mahusiano ya kidugu baina yao na kuondokana na dhana ya kudhani siasa ni uadui hasa katika kipindi hiki cha kampeni.

Alisema mdahalo huo utakaorushwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya redio vya mjini Iringa, utawawezesha wagombea hao kuelezea sera na mikakati yao katika kukuza pato la mkazi wa Iringa, ajira kwa vijana, kuboresha sekta za afya, miundombinu ya barabara, michezo na elimu.

Wagombea hao wanatarajia pia kuzungumzia namna wanatavyoshiriki kuboresha upatikanaji wa huduma bora ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango.

"Hii ni kuwataharifu kwamba wagombea wote pamoja na vyama vyao vimethibitisha kushiriki mdahalo huo na hivyo kutoa fursa adimu kwa wahahabari kushiriki katika mchakato wa kuwasaidia wananchi kupata viongozi bora," alisema.

Alisema hakuna mgombea atakayeruhusiwa kutumia lugha za kejeli, matusi au za aina yoyote ile zinazoshusha utu au hadhi ya mtu ili kuwawezesha wagombea hao kujikita kwenye hoja za msingi.

Wakati huo huo, Leonard amewasihi wanahabari kurudi kwenye misingi ya taaluma na kuzingatia miiko ya uandishi wa habari za uchaguzi ili kuirejeshea heshima yake tasnia hii.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment