Sunday, 4 October 2015

WALEMAVU KILOLO WAUPONGEZA MPANGO WA TASAF WA KUSAIDIA KAYA MASIKINIWALEMAVU wawili wa wilayani Kilolo mkoani Iringa, wanaodai kutengwa na familia zao, wameipongeza awamu ya tatu ya mpango wa TASAF wakisema imewaongezea pumzi katika maisha yao yaliyokuwa hayatabiriki.

Walemavu hao, Maila Magilanga (30) ambaye ni mlemavu wa miguu na Julius Kadinde (23) ambaye ni mlemavu wa ngozi wanaishi katika kijiji cha Lulanzi wilayani humo.

Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Kilolo, Venance Mwaikambo alisema walemavu hao ni sehemu ya kaya masikini 6,464 za wilaya hiyo ambao kwa kupitia mpango huo wanapata ruzuku ya msingi na ya masharti inayowawezesha kugharamia mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, afya na maji.

“Kwa kupitia mpango huo kaya hizo zinapokea msaada wa kati ya Sh 20,000 na Sh 70,000 kila baada ya miezi miwili, fedha zinazolenga kuboresha maisha yao kwa kupitia uwekaji akiba na uanzishaji wa shughuli za kiuchumi,” Mwaikambo alisema na kuzitaja baadhi ya shughuli hizo kuwa ni ufugaji wawanyama wadogo kama kuku, sungura na mbuzi.

Alisema katika awamu ya kwanza ya mpango huo, kaya hizo 6,464 zilipokea zaidi ya Sh Milioni 212.8 yakiwa ni malipo ya mwezi Julai na Agosti mwaka huu na awamu ya pili ya mwezi Septemba na Oktoba kaya hizo zililipwa mwishoni mwa wiki iliyopita zaidi ya Sh Milioni 200.

Akipokea awamu ya pili ya msaada huo juzi, Magilanga mzazi wa watoto watano anayepata Sh 40,000 kila baada ya miezi miwili alisema; “nilitengana na mume wangu baada ya kupooza miguu mwaka 2008. Baada ya kutengana naye, mimi na watoto wangu nilirudi kwa mama yangu mzazi tunakoishi mpaka sasa.”

Alisema kwa kupitia mpango huo wa TASAF na shughuli zake zingine ndogondogo anazofanya nyumbani kwa mama yake kwa kiasi wanamudu kupata mahitaji yao ya msingi kama chakula na matibabu.

Naye Kadinde anayepokea Sh 20,000 kila baada ya miezi 2 alisema; “nilitengwa na familia yangu baada ya kuzaliwa na ulemavu huu wa ngozi. Sehemu kubwa ya maisha yangu nimeishi na bibi kabla sijatafuta chumba changu cha kupanga na kuanza kujitegemea.”

Kadinde ambaye ulemavu wake ulisababisha ashindwe kupata elimu ambayo matokeo yake yamemfanya ashindwe kusoma na kuandika alisema kiasi hicho cha fedha kinamuwezesha kulipa kodi ya pango katika nyumba aliyopanga.

“Kwa mwezi nalipa Sh 6,000. Natamani kiasi kinachobaki kutoka katika fedha nayopewa na TASAF nikitumie kwa ufugaji wa kuku, lakini nashindwa kufanya hivyo kwasababu mazingira ya mahali napoishi hayaniruhusu,” alisema.

Alisema mbali na msaada huo amekuwa anafanya vibarua mbalimbali kijijini hapo ili apate kipato cha ziada kinachomuwezesha angalau kupata mlo mmoja kwa siku.

“Pamoja na hayo yote ndoto yangu ni kuona narudi shule na nipo tayari kuanza darasa la kwanza endapo nitapata msaada utakaoniwezesha kumudu mahitaji yangu muhimu ya kila siku,” alisema huku akiwasihi baadhi ya watu wanaomnyanyapaa kijijini hapo kuacha tabia hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment