Tuesday, 13 October 2015

MWENYEKITI WA UVCCM WILAYA YA KILOLO NA MJUMBE WAKE WATIMKIA CHADEMA, WASEMA MUDA WA MABADILIKO UMEWADIA

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Sifuni Makongwa leo ametangaza kukihama Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Pamoja na Makongwa mwingine aliyejitoa katika chama hicho na kujiunga na CCM ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Kilolo, Pendo Mpalanzi ambaye pia alikuwa Katibu wa makatibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa wilaya hiyo.

Kwa pamoja wamesema wamejitoa katika chama hicho na wanajiunga katika timu waliyoiita ya mabadiliko ya Ukawa ili waweze kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo kuleta mabadiliko ya kweli.

Akizungumza na wanahabari katika bustani ya manispaa ya Iringa, Makongwa alisema; “nimevumilia kwa muda mrefu lakini naona nafsi yangu inanisuta. Sijisikii tena kuendelea kuwa mwanachama wa CCM nikikumbuka jinsi mchakato wa kura za maoni ya ubunge ulivyokuwa na dosari.”

Alisema kura za maoni zilizorudiwa mara mbili na kumpa ushindi Venance Mwamotto dhidi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Profesa Peter Msolla ziligubikwa na udanganyifu mkubwa uliomsaidia mshindi huyo kuibuka kidedea katika marudio hayo.

Akiwalaumu viongozi wa chama wa wilaya hiyo, Makongwa alisema waliruhusu wana CCM na wasio wana CCM kushiriki katika kura za maoni za jimbo hilo kwa lengo la kumbeba mgombea mmoja; jambo lililowanyima haki wagombea wengine.

“Siku kadhaa kabla ya mchakato wa kura za maoni zilitolewa kadi mpya bila utaratibu na zilitolewa kwa watu ambao hawakuwa na nia ya kuwa wanachama wetu ili kumbeba mgombea fulani,” alisema.

Alisema atahakikisha wanafanya kampeni ya nguvu katika siku zilizobaki ili mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Bryan Kikoti apate ushindi wa kishindo.

Naye Mpalanzi alisema; “ni ngumu kuwa huru ndani ya CCM wilayani humo kama viongozi wake wa chama wilaya, wataendelea kuwa viongozi.”

Bila kuwataja majina, alisema viongozi hao ni watu wanaoendekeza makundi, majungu, fitina na kila aina ya hila kwa watu ambao hawaungi mkono hoja zinazolenga kuwanufaisha wao.

“Mimi Pendo kwa akili zangu timamu, bila kushawishiwa na mtu yoyote leo nimeamua kuondoka CCM na kujinga na timu ya Ukawa kwa kupitia Chadema ili nishirikiane na wana Kilolo wengine kuyatafuta na kuyapata mabadiliko ya kweli,” alisema.

Alisema Kilolo inahitaji mbunge mwenye maono na kwa mtazamo wake mgombea mwenye sifa hiyo kwasasa ni Kikoti.

Akiwapokea wanachama hao, Kikoti alisema; “naamini hajanifuata mimi, ni wana Kilolo kama walivyo wana Kilolo wengine wenye kiu ya mabadiliko ambayo kwa vyovyote vile haiwezi kupatikana kupitia CCM.”                                                                                               

Reactions:

0 comments:

Post a Comment