Monday, 12 October 2015

MWAKALEBELA, MSIGWA WASHIRIKI MDAHALO WA WAGOMBEA UBUNGE JIMBO LA IRINGA MJINIWAGOMBEA wanne kati ya sita wanaowania ubunge wa jimbo la Iringa Mjini wamechuana vikali katika hoja ya uchumi na ajira katika mdahalo ulifanyika mjini Iringa juzi kwa uratibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC).

Wagombea hao Frederick Mwakalebela wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), Daudi Masasi wa ADC na Robert Kisinini wa Democratic Party (DP) walishiriki mdahalo huo uliovuta zaidi hisia za vyama vyenye wafuasi wengi zaidi vya CCM na Chadema.

Mwenyekiti wa IPC, Frank Leonard alisema mgombea wa ACT Wazalendo Chiku Abwao na wa Chausta, Paulina Mgimwa hawakufanikiwa kuhudhuria mdahalo huo uliolazimika kusitishwa dakika 15 kabla ya muda wake kwisha baada ya wafuasi wa Chadema na CCM kuanza vita ya maneno kila wagombea wao walipokuwa wakiongea.

Wakati Abwao alikuwa safarini kuelekea Arusha kwa ajili ya kushiriki mazishi ya aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia ACT Wazalendo, Estomih Malla, Mgimwa kwa upande wake Mgimwa hakutokea wakati wa mdahalo huo pamoja na kuahidi kushiriki.

Mdahalo huo ulioanza kwa kila mgombea kutumia dakika 5 kueleza wasifu wake, sababu ya kugombea na vipaumbele vyake endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Iringa Mjini, ulimalizika salama katika ng’we hiyo kwa wagombea hao kujieleza kwa ufasaha.

Kila walipopata nafasi wagombea hao walijinadi kwa kuvitofautisha vyama vyao wakidai vina sera nzuri zinazolinda wawekezaji wakiwemo wa ndani na zina mikakati inayolenga kuziboresha sekta za uchumi kama viwanda, biashara, kilimo na michezo ili zitoe nafasi nyingi za ajira.

Wakati Mwakalebela akielezea mengi mazuri yaliyofanywa na serikali ya CCM kwa miaka mingi na kwamba inastahili kuendelea kuaminiwa na wananchi kwa kuwa ina sera nzuri na dhamira ya dhati ya kushughulikia kero za wananchi, wagombea wa vyama vya upinzani walisema nchi inahitaji sera mbadala ili kukuza sekta hizo.

Joto la mdahalo huo wa kwanza kufanywa katika historia ya IPC lilianza kupanda kila mara mgombea wa CCM na Chadema walipokuwa wakipata fursa ya kuzungumza.

Wafuasi wa vyama hivyo walikuwa wakishangilia mara kwa mara kila wagombea wao walipokuwa wakiongea jambo lililoonekana kukasirisha upande mwingine ambao nao ulijikuta katika mazingira ya kutaka kujibu.

Hali ilikuwa mbaya dakika 15 kabla ya mdahalo kumalizika baada ya Mchungaji Msigwa kutaka kupuuza swali lililomtuhumu kutaka kukwamisha miradi ya barabara za mjini Iringa inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Pamoja na changamoto hiyo, wadau wa maendeleo mjini Iringa wameipongeza IPC kwa kuandaa mdahalo wakisema umewawezesha wagombea hao kukutana katika meza moja na kujadili maendeleo ya jimbo la Iringa Mjini kwa mara ya kwanza tangu waanza kampeni zao.

“Tuipongeza IPC kwa kazi kubwa waliyofanya, kwa kweli vilabu vya waandishi katika mikoa mingine vingeiga suala hili vingesaidia sana kuwawezesha wananchi kupata chaguo sahihi katika uchaguzi mkuu,” alisema Hamis Malinga.

Malinga aliungana na wadau wengine kwa kuitaka IPC kuandaa mdahalo mwingine siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment