Tuesday, 6 October 2015

MWAKALEBELA APONGEZWA KWA KUENDESHA KAMPENI ZA KIUNGWANA


MGOMBEA ubunge jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Frederick Mwakalebela amepongezwa na wapiga kura wa mjini Iringa kwa kufanya kampeni za kistaarabu.

Tangu azindue kampeni yake Septemba 6, mwaka huu, Mwakalebela amekuwa akijielekeza katika kufafanua Ilani ya CCM na mambo atakayofanya endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Tofauti na baadhi ya wagombea, Mashaka Kikoti alisema; “Mwakalebela huwezi msikia akimtusi au kumkejeli mgombea mwingine.”

Naye Johnson Kimbe alisema; “ukianza kumsikiliza Mwakalebela huwezi kuchoka kwasababu mwanzo mwisho anaeleza mipango yake inayolenga kumaliza kero za wananchi wa jimbo hili la Iringa Mjini.”

Kimbe alisema amemsikiliza Mwakalebela na alichojifunza kutoka kwake ni kwamba hana muda wa kuwajadili wagombea wenzake kwa kutumia lugha zinazohudhi au zinazowashushia hadhi wagombea wenzake.

Akihutubia wananchi waliojitokeza katika mkutano wake uliofanyika juzi katika stendi ya mabasi yaendayo mikoani ya mjini Iringa alisema anayafahamu matatizo yaliyopo katika sekta mbalimbali jimboni humo na akaahidi kuyafanyia kazi kwa weledi na umakini mkubwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Nayajua matatizo katika sekta ya afya, elimu, biashara, miundombinu na nyingine, nichaguweni niwe mbunge wenu ili niwaoneshe namna mbunge anavyotakiwa kuyafuatilia na kuyafanyia kazi matatizo ya watu wake,” alisema.

Alisema CCM haikukosea kumpa ridhaa ya kugombea ubunge katika jimbo hilo kwani analindwa na rekodi zake nzuri katika maeneo mengi ambayo amafanya kazi ya kuwatumikia watu.

“Mnajua jinsi nilivyoshiriki kukuza soka la Tanzania nilipokuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, mnajua kazi kubwa nilizofanya kwa kipindi kifupi tu baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Wangong’ombe na mnajua rekodi zangu katika maeneo mengine niliyofanya kazi,” alisema.

Alisema rekodi nzuri ya kuwapenda na kuwatumikia watu katika maeneo mbalimbali inampa sifa ya ziada ya kuwa mbunge wa jimbo hilo tofauti na wagombea wa vyama vingine.

Mbali na Mwakalebela, wengine wanaogombea jimbo hilo ni aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), aliyekuwa mbunge wa viti maalumu mkoa wa Iringa, Chiku Obwao (Chadema) ambaye anawania jimbo hilo kupitia chama cha ACT Wazalendo na Daudi Masasi anayegombe a kupitia chama cha ADC.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mtazamo wa watu wa Iringa katika kujiletea maendeleo ulibadilika na kuwa wa vurugu, lawama na maandamano ya kupinga pia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali.

Alisema watu wa Iringa wanatakiwa kuondokana na mtazamo huo kwa kumchagua yeye kuwa mbunge, madiwani wa kata zote za manispaa hiyo na mzee wa hapa kazi tu, Dk John Magufuli anayewania urais kupitia chama hicho kikongwe nchini.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment