Saturday, 26 September 2015

YANGA YAIFUNGA SIMBA 2-0


Mabingwa wa soka nchini Yanga leo imefuta uteja kwa watani wake wa jadi Simba baada ya kufanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Taifa.
Alikuwa ni Amis Tambwe aliyeanza kupeleka kilio msimbazi kwenye dakika ya 44 baada ya kufunga goli safi akitumia guu la kushoto kumalizia kazi nzuri ya Malimi Busungu.
Simba iliweza kuwadhibiti Yanga kipindi chote cha kwanza, walitengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na Hamis Kiiza, mchezaji wa zamani wa Yanga, ilikosa umakini.
Hadi mapunziko Yanga ilitoka kifua mbele kwa bao hilo moja.
Kipindi cha pili Yanga iliuanza mchezo huo kwa kasi na walifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 79 kupitia kwa Malimi Busungu.
Busungu alifunga bao hilo akimalizia kazi nzuri ya Mbuyu Twite aliyerusha mpira kona ambao uliparazwa na Haruna Niyonzima kabla ya kumfikia Busungu.
Baada ya kupachika bao hilo la pili, Yanga walicheza mchezo wa kujihami na kupoteza muda ambapo ilipelekea Twite kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kupewa kadi ya pili ya njano.
Mwamuzi wa mpambano huo Israel Mujuni aliongeza dakika 8 za nyongeza hata hivyo Simba ilishindwa kupata walau bao la kufutia machozi.
Kwa matokeo hayo Yanga imejikita kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Vodacom baada ya kushinda michezo yake yote.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment