Saturday, 26 September 2015

WANAFUNZI WA ZAMANI LUGALO SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA UZIO WA SHULE

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi Waliosoma Lugalo Sekondari ya Iringa mwaka 1990, Faraja Chang'a (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa sekondari hiyo, Benjamin Kabungo sehemu ya mifuko 200 ya saruji walioitoa kusaidia ujenzi wa shule hiyo
Baadhi ya wanafunzi hao wakiwa katika picha ya pamoja 

WANAFUNZI waliosoma na kumaliza elimu yao ya sekondari katika shule ya sekondari Lugalo ya mjini Iringa wanazidi kujitokeza na kuipiga jeki shule hiyo ili kuboresha mazingira yake.

Katika tukio la juzi, wanafunzi 43 waliomaliza kidato cha nne shuleni hapo mwaka 1990 walichangia mifuko 200 ya saruji (sawa na tani 10) ili itumike kusaidia ujenzi wa uzio wa shule hiyo.

Akikabidhi msaada huo mbele ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi hao wa mwaka 1990, Faraja Chan’ga alisema; “msaada huu una thamani ya Sh 2, 560,000.”

Alisema mbali na shughuli zingine za kimaendeleo zitakazokuwa zikifanywa na umoja huo ambao uanachama wake upo wazi kwa wanafunzi wote waliomaliza shuleni hapo mwaka 1990, mpango wao ni kusaidia maendeleo ya shule hiyo ambayo ni chimbuko la maendeleo yao kila watakapopata fursa.

Mmoja wa wanafunzi hao wa mwaka 1990, Zakayo Mleduka alisema; “tunawiwa kuchangia maendeleo ya shule hii kwasababu mafanikio yetu yanatokana na shule hii. Tulisoma hapa shule ikiwa na majengo mazuri na walimu wa kutosha. Leo hayo yote hayapo, kwa kidogo tunachopata tunaweza kusaidia kubadili hali hiyo.”

Akishukuru kwa msaada huo, Mkuu wa shule hiyo, Benjamin Kabungo alisema wazo la kujenga uzio wa shule hilo linalenga kudhibiti vitendo vya uhalifu na wizi wa mali mbalimbali za shule kutokana na ongezeko la watu wanaokatiza katika viunga vya shule hiyo.

“Tuliweka malengo kwamba kila mwaka tujenge mita 10 za uzio. Na katika kufikia lengo hilo kila mwanafunzi anayeingia kidato cha kwanza na cha tano anachangia Sh 10,000,” alisema na kuahidi umoja wa wanafunzi hao kwamba msaada huo utatumika kwa lengo lililokusudiwa.

Alisema hadi kukamilika kwake, uzio huo utakaokuwa na urefu wa mita 1,500 utagharimu Sh Milioni 140.8 hadi kukamilika kwake na kwamba mpaka sasa mita 200 zimekwishajengwa huku zikitumia zaidi ya Sh Milioni 93.

Msaada wa wanafunzi hao wa mwaka 1990, unakuwa wa pili kutolewa katika shule hiyo na makundi yanayoundwa na wanafunzi waliomaliza shuleni hapo.

Mei 4, mwaka huu, wanafunzi 37 walioanzisha kampuni ijulikanayo kama Lugalo Associates Company Ltd walitumia zaidi ya Sh Milioni 3.5 kukarabati nyumba chakavu ya mkuu wa shule hiyo.

Baada ya ukarabati huo, Katibu wa kampuni hiyo, Joyce Thomas alisema kampuni yao inaendelea kutafuta fedha nyingine kwa ajili ya kukarabati nyumba nyingine nne za walimu, shuleni hapo.

Alisema fedha wanazotumia kuikumbuka shule hiyo inatokana na jasho lao wenyewe na misaada kutoka kwa wadau wao.


Pamoja na kusaidia kuboresha mazingira ya shule hiyo, kampuni hiyo imeahidi pia kutoa zawadi kwa wanafunzi bora wa wa kidato cha kwanza hadi cha sita, kila mwaka kuanzia mwaka huu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment