Saturday, 19 September 2015

USAID YAIFUNGULIA MILANGO KLABU YA WANAHABARI MKOA WA IRINGASHIRIKA la Misaada la Marekani (USAID) limefungua ukurasa wa ushirikiano na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa (IPC) ambao kama utafanikiwa utaiwezesha klabu hiyo kuweka historia nyingine ya maendeleo kwa wadau wake nchini.

IPC ni klabu ya kwanza nchini kuanzisha jarida ambalo mbali na kuchapisha mambo mbalimbali yahusuyo afya, limekuwa likitoa elimu ya Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Jarida hilo lililokuwa likisambazwa bure katika kata zote za mkoa wa Iringa na Njombe, lilikuwa likipata ufadhili kutoka Shirika la Kimataifa la Forum Syd la Sweden na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Ukimwi (TACAIDS) kati ya mwaka 2004 na 2008.

Katika majadiliano yao yaliyofanyika hivikaribuni katika ofisi za IPC zilizopo mjini Iringa kwa kuhusisha uendelezaji wa jarida hilo, IPC iliwakilishwa na Katibu Mtendaji  Tukuswiga Mwaisumbe, Mweka Hazina Selemani Boki na Mratibu wa IPC Ester Kipala.

USAID walioambatana na maafisa wawili kutoka Institute for Parliamentary Support in Africa (IPSA), Kimberly Smiddy na Kevin Sudi, waliwakilishwa na Daniel Pearf na Jim Jim.

Katibu Mtendaji wa IPC aliwaambia wawakilishi hao kwamba:  “Kwa kupitia Jarida letu la Mkombozi, wanahabari wa mkoa wa Iringa walishiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya VVU, Ukimwi na afya ya jamii na baada ya kukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha ushiriki wetu ulipungua.”

Mwaisumbe alisema wananchi, hasa wale wa vijijini ambao sio rahisi kufikiwa na vyombo vingine vya habari kama magazeti, redio na televisheni walilitumia jarida hilo kupata taarifa mbalimbali zinazohusu mambo hayo kutoka ndani na nje ya jamii inayowazunguka na hivyo kuchukua tahadhari.

Akiomba msaada kutoka USAID, Boki alisema, IPC imekuwa ikipokea maombi ya kuendelea kusambaza jarida hilo vijijini lakini uhaba wa fedha umesababisha kwa muda mrefu lisizalishwe.

Pamoja na kuwepo kwa kiu kubwa ya kumaliza kilio cha wananchi hao, Mwaisumbe alisema IPC ingependa kuona katika mipango yake ya baadaye inakuwa na redio yake ya kijamii itakayofanya kazi kubwa ya kutoa elimu ya afya kwa watu wa mkoa wa Iringa na mikoa jirani.

Akijibu maombi hayo, Jim aliwataka IPC kuyawakilisha kwa maandishi ili fedha zitakapopatikana na miradi hiyo kukubaliwa iingizwe katka kundi la miradi inayofadhiliwa moja kwa moja na USAID.

“Leteni maombi yenu na mnapoyaleta ni muhumi mkafahamu kwamba sisi sio wenye mamlaka ya mwisho ya maombi hayo. Tutakachofanya ni kuyafikisha kwa wanaohusika ili yafanyiwe kazi,” alisema.

Endapo mpango huo utafanikiwa, Mwaisumbe alisema IPC itaandika historia nyingine ya kuwa na miradi itakayohusisha jamii inayowazunguka.

“Mipango yetu ni kuona tunashiriki kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya afya, ikiwemo eneo la afya ya mama na mtoto, uzazi wa mpango na VVU na Ukimwi,” alisema.

Mengine yaliyojadiliwa na taasisi hizo mbili ni pamoja na mambo yanayohusu ushirikiano baina ya sekta za umma na binafsi, utawala bora na maadili ya viongozi wa umma.

USAID na IPSA walitaka kujua kama wanahabari wamewahi kupata mafunzo katika maeneo hayo na yoyote kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na changamoto zinazowakabili katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.

Pamoja na kutembelea ofisi kuu ya IPC, wageni hao walipata fursa pia ya kutembelea mradi klabu hiyo ujulikanao kwa jina la IPC Development Facility.

Kwa kupitia mradi huo, IPC inasambaza vifaa vya maofisini, intoa huduma za uchapishaji, internet, ukodishaji wa kamera kwa ajili ya shughuli mbalimbali na inaendesha mradi wa kuweka na kukopa (IPC Vicoba) ambao lengo lake ni kuwakopesha wanachama wake ili wafanikishe shughuli zao mbalimbali.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment