Saturday, 19 September 2015

MWAKALEBELA AWAPIGIA MAGOTI WALIOIKIMBIA CCM 2010

MGOMBEA  ubunge  wa  jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama  cha Mapinuzi (CCM), Frederick  Mwakalebela

MGOMBEA  ubunge  wa  jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama  cha Mapinuzi (CCM), Frederick  Mwakalebela amewapigia magoti waliokuwa wapenzi na wanachama wa chama hicho waliojitoa CCM mwaka 2010 na kuwapigia kura wapinzani, akiwaomba warudi kundini kwani kiu yao ya maendeleo inakwenda kutimia baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba , mwaka huu.

Makada hao walijitoa CCM na kumuunga mkono mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ikiwa ni matokeo ya hasira walizokuwanazo baada ya CCM kumkata Mwakalebela katika kinyang’anyiro hicho cha mwaka 2010 pamoja na kwamba alishinda kura za maoni za ubunge za jimbo hilo.

Uamuzi wa makada hao wa CCM kumtosa mgombea wao wa CCM, Monica Mbega ulimuwezesha Mchungaji Msigwa kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.

Akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa soko kuu mjini Iringa, Mwakalebela alisema; “natambua jinsi uamuzi ule ulivyowaumiza wana CCM na wapenzi wengi wa chama chetu na hivyo kuamua kutoa kura zao kwa mgombea wa upinzani.”

Alisema anatambua pia jinsi wananchi wa Iringa walivyopoteza muelekeo wa kimaendeleo katika kipindi chote ambacho Mchungaji Msigwa amekuwa mbunge wa jimbo la Iringa Mjini na akawataka hayo yote wayasahau kwani amepata fursa itakayomaliza kilio chao endapo atachaguliwa kuwa mbunge wao katika uchaguzi huo.   

“Ili kumaliza kabsa hasira zenu mnayo kazi moja tu ifikapo Oktoba 25, na kazi hiyo si nyingine, ni ya kumpigia kura mgombea wetu urais Dk John Magufuli, mimi mwenyewe na madiwani wote kutoka CCM ili tulete maendeleo,” alisema.

Alisema uamuzi huo ukifanywa, utatoa fursa kwa jimbo la Iringa Mjini kuzaliwa upya na kurejesha hadhi na heshima yake ya kimaendeleo iliyosimama kwa miaka mitano.

Mwakalebela alisema anafahamu kazi kubwa iliyoko mbele yake endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo na akaahidi kuifanya kwa weledi mkubwa.

“Nayajua watu wa Iringa wanahitaji nini katika sekta ya afya, elimu, miundombinu, kilimo, biashara, makundi maalumu, maji na huduma nyingine muhimu,” alisema na kuomba kura ili azishughulikie changamoto zilizopo katika sekta hizo kwasababu anafahamu wapi kwa kuanzia.

Akiwaahidi wafanyabiashara wa soko hilo alisema atahakikisha hawabugudhiwi bila sababu za msingi ili wafanye biashara zao katika mazingira yatakayoamsha upya ushirikiano wao mzuri na mamlaka zingine za serikali.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu aliyekuwa mshindi wa pili katika kura za maoni za jimbo hilo, alijitokeza katika mkutano huo na kuwahakikishia wanaCCM na wapenzi wengine wa chama hicho kwamba; “tumevunja makundi, kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kutafuta ushindi wa chama chetu na wagombea wake wote.”

Msambatavangu alisema wananchi wa jimbo la Iringa Mjini wanataka maendeleo na mtu  pekee  wa  kuwaletea maendeleo wanayoyataka ni Mwakalebela.

Msambatavangu anayekumbukwa na wengi kwa jinsi alivyoonesha mapenzi yake ya kisiasa kwa Waziri Mkuu aliyejiudhuru, Edrward Lowassa wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM, alimnadi pi mgombea urais wa tiketi ya CCM, Dk Magufuli akisema ana dhamira ya dhati ya kubadili muelekeo wa taifa hili, kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment