Sunday, 13 September 2015

MKOA WA IRINGA WAADHIMISHA WIKI YA USALAMA BARABARANI


JESHI la Polisi Mkoani Iringa limeishauri serikali kuanzisha mtaala wa elimu ya usalama barabarani katika shule za msingi, sekondari na vyuo ili kufanikisha kauli mbiu ya Rais Jakaya Kiwete ya kuwa Tanzania Bila Ajali Inawezekana.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Iringa (RTO), Leopord Fungu kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoani hapa, yaliyofanyika katika viwanja vya stendi kuu ya mabasi, mjini Iringa.

Pamoja na pendekezi hilo, Fungu alisema ili kupunguza ajali za barabarani ni muhimu sheria ya usalama barabarani na ile ya usafirishaji zikapitiwa upya ili adhabu kali zitolewe kwa madereva wanaozikiuka.

Akitoa takwimu ya tathmini ya ajali kwa kipindi cha Januari hadi Julai 2014 na 2015, alisema wakati mwaka 2014 kulikuwa ajali 91, mwaka huu zilikuwa 75, huku zilizosababisha vifo zikiwa 74 kwa 58 na za majeruhi 17 kwa 17.

Alisema wakati watu 81 walikufa katika ajali hizo mwaka 2014, watu 143 walipoteza maisha mwaka huu huku majeruhi katika kipindi hicho wakiwa 49 kwa 113.

Akizungumzia ajali za pikipiki (bodaboda) katika kipindi hicho, Fungu alisema zimepungua kutoka 39 mwaka jana hadi 17 mwaka huu huku waliokufa katika ajali hizo nayo ikipungua katika kipindi hicho kutoka 23 hadi 16.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi ametoa onyo kali kwa madereva  wa vyombo  vya  usafiri, hususani katika kipindi hiki cha kampeni  za uchaguzi akiwataka kuzingatia sheria ili kampeni hizo zimalizike salama.

“Katika kipindi kama hiki, shughuli za matumizi ya barabara ni kawaida kuongezeka. Wapo wanaojisafirisha au kusafirishwa kwa ajili ya kushiriki shughuli za kisiasa, kwahiyo ni muhimu wakazingatia sheria,” alisema.
 
Kwa  upande wake Mwenyekiti  wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa  wa Iringa,  Salima Asas alisema  kumekuwepo na ongezeko la walemavu wa viungo wanaotokana na ajali hasa baada ya kushamiri kwa usafiri wa bodaboda.


“Baadhi ya madereva wa bodaboda hawana mafunzo na tunahuhudia jinsi biashara yao inavyoogopesha kwa ajali nyingi,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema wakati serikali ikipokea mapendekezo hayo, jeshi la Polisi linatakiwa kuendelea kushirikiana na wadau wake kudhibiti ajali hizo za barabarani.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment