Wednesday, 9 September 2015

MCHUNGAJI MSIGWA KUZINDUA KAMPENI ZAKE ZA UBUNGE IRINGA MJINI JUMAPILI, AAHIDI KAMPENI ZA KISTAARABUWIKI moja baada ya Mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM), Frederick Mwakalebela kuzindua kampeni zake kwa kishindo katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa atazindua kampeni zake Jumapili, Septemba 12.

Wakati kampeni za Mwakalebela zilisindikizwa na viongozi mbalimbali wa CCM ngazi ya wilaya na mkoa, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Yamoto bendi na wasanii wa Bongo Movies akiwemo Irine Uwoya, Blandina Chagula (Johari), Single Mtambalike (Richie) na Jacob Steven (JB) na Dude;

Mchungaji Msigwa amesema uzinduzi wa kampeni zake utakuwa tofauti kabisa na ule wa CCM kwani mbali na kutoleta msaani yoyote kutoka nje ya mkoa, hakuna kiongozi yoyote wa kitaifa atakayemsindikiza.

“Mimi na timu yangu ya kampeni tunataka kukutana na wapiga kura wetu bila kutumia makundi ya wasanii na niahidi kwamba tutafanya kampeni za kistaarabu tofauti kabisa na za wenzetu wa CCM,” alisema.

Alisema katika mkutano huo wa uzinduzi wataeleza kazi walizofanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,  na mikakati yao ya kuwaletea maendeleo watanzania katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya mabadiliko chini ya Edward Lowassa.

Aliwaomba wananchi wapenda maendeleo na mabadiliko kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa stendi ya mabasi yaendayo vijijini, Mlandege mjini kujitokeza kwa wingi kusikia pia sera zao na majibu ya hoja mbalimbali zinazotolewa na wapinzani wao CCM.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment