![]() |
Matokeo ya utafiti wa Twaweza kuhusu Uchaguzi Mkuu yamepingwa na
wasomi, wanaharakati na wanasiasa, akiwamo mgombea urais wa Chadema na Ukawa,
Edward Lowassa ambaye ameuponda na kueleza kuwa matokeo halisi yatapatikana
Oktoba 25.
Utafiti
huo unaonyesha kuwa kama kura zingepigwa kati ya Agosti na Septemba, mgombea wa
CCM, Dk John Magufuli angeibuka na ushindi wa asilimia 65, wakati Lowassa angepata
asilimia 25.
Lakini
wadau waliohojiwa na Mwananchi jana wamesema utafiti huo haujaakisi hali halisi
inavyoonekana kwenye mikutano ya kampeni, ambayo inaonyesha wawili hao
wanachuana vikali kutokana na kukusanya mashabiki wengi.
“Watanzania
tusipumbazwe na tafiti ambazo hatujashiriki. Tushiriki kwa mafuriko Oktoba 25,
majibu ya kweli tutayapata,” alisema Lowassa kwenye akaunti yake ya twitter.
Kwenye
mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Ndanda jana, ikiwa ni muda mfupi baada
ya Twaweza kutangaza matokeo ya utafiti huo, Lowassa alisema anashangazwa kwa
kuwa wananchi wanaomuunga mkono ni wengi.
“Kuna
utafiti wa kura ya maoni umetolewa ukisema eti Magufuli amepata asilimia 65 na
mimi 25. Nawashangaa kwa kuwa wanaoniunga mkono wako wengi,” alisema Lowassa na
kuwaoji wananchi wangapi watampigia kura katika uwanja huo.
Huku
wakishangilia wananchi hao walimjibu Lowassa “Tutakupigia” huku wakinyoosha
mikono juu.
Baadaye
Lowassa alisema: “Tutawajibu kwenye kura tarehe 25 na hamuwezi kukosea kwa kuwa
mnaziona mvi hizi. Nangojea mafuriko ya kura kutoka kwenu.”
Lowassa
alijiondoa CCM baada ya jina lake kuenguliwa na Kamati Kuu na kujiunga na
Chadema Julai mwishoni. Chama hicho kilimpa fursa ya kugombea urais, akiungwa
mkono na vyama vingine vya NLD, NCCR-Mageuzi na CUF vinavyounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa).
Maoni
ya wadau
Mbali
na Lowassa kutokubaliana na matokeo ya utafiti huo, wadau walioongea na Mwananchi
pia walionyesha kuupinga.
Mwenyekiti
wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama alisema matokeo
ya utafiti wa Twaweza hayalingani na hali halisi ya kisiasa inavyoendelea
nchini.
“Kile
kinachoonekana huko nje ni picha mbili tofauti,” alisema Profesa Mlama.
Alisema
licha ya kwamba Twaweza wamefanya utafiti huo kwa kutumia vigezo vyao, matokeo
yasingeonyesha tofauti kubwa kati ya wagombea hao.
Kauli
hiyo iliungwa mkono na Profesa Kitila Mkumbo ambaye alisema: “Matokeo halisi
tutapata baada ya wananchi kupiga kura Oktoba 25.”
Wakati
wadau hao wakizungumzia tofauti ya uhalisia wa hali ilivyo na matokeo ya
utafiti, mhadhari wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Loisulie aliwataka
wapinzani kutopuuzia maoni hayo ya wananchi, hasa kutoelewa nafasi ya Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Wanaweza
wakapuuzia utafiti huo kwa kuwa unampa ushindi Dk Magufuli, lakini sio hili la
Ukawa si chama cha siasa kilichosajiriwa kwa sababu itakapofika Oktoba 25 watu
wanaweza kwenda kwenye karatasi ya kupigia kura kutafuta Ukawa,” alisema.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema licha ya kukosa
uhalisia kwa hali ya kisiasa iliyopo, matokeo hayo yanaweza kuwa changamoto kwa
Ukawa, kujipanga upya na kuangalia mbinu za kuongeza ushawishi kwa siku
zilizobakia.
Hata
hivyo, Mbunda alisema matokeo hayo hayawezi kutabiri ushindi wa urais kati ya
Dk Magufuli na Lowassa.
“Haileti
mantiki kwa mashabiki wa Lowassa halafu utafiti uonyeshe amepata asilimia 25 ya
kura. Ningependa ufanyike utafiti mwingine ili kuondoa maswali yaliyopo kwa
sasa,” alisema.
Wakili
wa kujitegemea na makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdalah Safari alisema
matokeo hayo ya Twaweza ni sehemu ya CCM kutapatapa na utafiti a;iouita “feki
na wa kutengeneza”.
Profesa
Safari alisema haiingii akilini, muungano wa Ukawa na Lowassa ukatoa asilimia
25.
“Nusu
ya vijana tumeshiriki kampeni za kuhakikisha wanajiandikisha kupiga kura na
hata utafiti wetu unaonyesha CCM watashindwa. Kwa hivyo wanatafuta kurubuni
taasisi ziwatengenezee uhalali wa kukubalika,” alisema Profesa Safari.
Maoni
kama hayo yalitolewa na Profesa Gaudence Mpangalla kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha
ambaye alisema ni matokeo ya propaganda za CCM.
Alisema
Lowassa akiwa CCM, matokeo ya utafiti wa taasisi hiyo yaliyonyesha alikuwa
anaongoza kwa ushawishi katika nafasi ya urais.
“Nina
shaka na hiyo methodolojia waliyoitumia kwa kweli,” alisema Profesa Mpangalla.
Dk
James Jesse, mhadhiri wa UDSM, Kitivo cha Sheria pia alikuwa na shaka na
utafiti huo.
“Matokeo
haya yanaonesha walihoji watu fulani walioandaliwa na hawakuhoji watu
mchanganyiko,” alisema.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku), Stephen Mwakajumulo alisema kama
Twaweza iliweka vigezo sahihi vya utafiti, basi upo uwezekano wa majibu kuwa
sahihi.
“Kumbuka
mwaka 2005 ilifanya utafiti wa aina hiyo na kueleza kwamba mgombea wa CCM Rais
Jakaya Kikwete angeshinda kwa asilimia 80 na matokeo yake yakawa kweli,’’
alisema na kuongeza mara nyingi utafiti unafanyika ili kutafuta mwelekeo wa
ukweli kwa kutumia vigezo muhimu.
Wanasiasa
Mgombea
ubunge wa Jimbo la Bumbuli (CCM), January Makamba alilalamika kuwa utafiti huo
umewapunguzia asilimia za ushindi kwani wanaamini itakuwa zaidi ya asilimia 65.
“CCM
haishangazwi na matokeo hayo kwa sababu, Magufuli amefika maeneo ya vijijini
zaidi kuliko mgombea yeyote, ameeleza sera zinazoeleweka na ana sifa za
uadilifu lakini wanaojadili mabadiliko hawaendani na historia yao, mwonekano
wao ndiyo sababu wananchi wamekatishwa tamaa na hoja zao,” alisema ambaye wiki
iliyopita alitangaza matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ambayo hakuitaja
unaoonyesha kuwa Magufuli anaongoza kwa asilimia 69.
“Mafuriko
ya (mgombea wa NCCR-Mageuzi mwaka 1995) Agustine Mrema na (mgombea wa Chadema
2010) Dk Willibrod Slaa hayajawahi kutokea hadi sasa. Haya yanayojitokeza kwa
Lowassa badala ya kuwasaidia yanawadhalilisha kwa kuwa mgombea wao hana uwezo
hata wa kujieleza jukwaani kwa hivyo matokeo hayo yanaakisi ukweli wa hali
halisi iliyopo...sasa wanaopinga na wao waje na utafiti wao tuone.”
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kabla ya kuzungumzia utafiti huo wataujadili
kwa kina kuangalia mazingira yaliyotumika kuufanya.
“Kwanza
tuone ulivyofanyika ndiyo tutatolea ufafanuzi,” alisema.
Katibu
Mkuu wa chama cha Sauti ya Wananchi (Sau), Ali Kaniki alisema matokeo hayo
hayawezi kuaminika kwa asilimia kubwa.
“Kuna
taasisi Uingereza walifanya utafiti kama huo na chama cha Labour Party
kilioneokana kuongoza sana, lakini hadi matokeo yanatangazwa kilianguka
vibaya,” alisema.
“Lakini
inatakiwa kuheshimu utafiti huo na tusidanganyike na hoja za mafuriko.
Wanaojitokeza kwenye mafuriko siyo wote wanaopiga kura.”
Hata
hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muhabi alisema matokeo
hayo ni chanzo cha kuashiria hatari ya machafuko, hivyo kusingekuwa na sababu
ya kutoa utafiti huo kwa muda mfupi uliosalia.
“Ukiangalia
ndani yake kuna propaganda za kisiasa zinazochezwa na CCM na inaweza kutuletea
shida. Watu wako kwenye presha sana nadhani ingekuwa sahihi kusubiria uchaguzi
ufanyike tu.”
Mwenyekiti
wa UDP mkoani Dar es Salaam, Joachimu Mwakitinga alisema hakuna uhusiano wa
hali halisi na matokeo ya asilimia 65 kwa Magufuli. Mwakitinga ambaye ni mjumbe
wa Kamati ya Mamlaka na Taratibu za Uendeshaji Uchaguzi, alisema matokeo hayo
ni uchochezi wa kampeni unaoweza kusababisha madhara makubwa kwenye Uchaguzi
Mkuu.
Wanaharakati
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Dk.Hellen Kijo-Bisimba
alisema sampuli iliyotumika kwa matokeo ya utafiti huo inaweza kuwa imeathiriwa
na mazingira ya maeneo husika. “Wakati mwingine sampuli inaweza kudanganya na
kuwa tofauti kabisa na uhalisia wa hali ilivyo na wakati mwingine kuelezea
uhalisia wenyewe.”
Mkurugenzi
wa Taasisi ya Sikika, Irinei Kiria alisema sampuli ya Watanzania 1,848 ni idadi
ndogo na isiyoakisi Watanzania milioni 23 wanaotarajiwa kupiga kura mwaka huu.
“Lakini
pia, wiki mbili tangu kufanyika uchaguzi huo ni muda unaoweza kubadili upepo
mkubwa wa kisiasa kwa hivyo haiwezi kuwa matokeo halisi kwa hali ya sasa.”
Kiria
alisema matokeo ya utafiti huo kwa Lowassa na Magufuli ni sawa na usiku na
mchana kutokana hali halisi ya kisiasa ilivyobadilika katika uchaguzi wa mwaka
huu.
Mratibu
wa Mtandao wa Watetezi za Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa
alisema matokeo na hali ya kisiasa nchini yanaonyesha tofauti kubwa.
Mwenyekiti
wa mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Arusha (Angonet), Petro
Ahham alisema utafiti ni mzuri, lakini pengo la ushindi wa CCM ni kubwa sana.
“Kwa
hali ilivyo sasa huwezi kusema kuna mshindi wa asilimia 65, labda tuelezwe
walioulizwa maswali ni waliojiandikisha tu sio hawa tunaowaona kwenye
mikutano,” alisema.
Mwanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Alline Ngirwa alisema utafiti huo
umeonyesha ni maeneo gani hasa ambayo wananchi wanakerwa, kwa hivyo utawasaidia
katika kipindi hiki wanapojiandaa kuamua.
“Wananchi
wanakerwa na huduma za afya, ukosefu wa maji na elimu duni. Kwa hiyo matokeo ya
utafiti huu yanatoa mwangaza kwa wapiga kura na wagombea juu ya vitu
wanavyohitaji kwenye serikali ijayo,” alisema Ngirwa.
Mkurugenzi
wa taasisi ya Compas Communication, Maria Salungi alisema utafiti huo si matokeo
ya uchaguzi na kwamba katika kipindi kilichobaki kuelekea Uchaguzi Mkuu,
yanaweza kubadilika.
“Haya
sio matokeo ya uchaguzi ni maoni ambayo yanaweza kubadilika kulingana na
wagombea watakavyoendelea kufahamika zaidi kwa wananchi, hivyo jamii isipokee kama
ndio matokeo halisi,” alisema
Alisema
katika utafiti huo, wengi waliohojiwa walitoa majibu kulingana na wagombea
kufahamika zaidi, kutokana na majina yao kutajwa mara kwa mara ikiwemo kwenye
vyombo vya habari na mabango.
Alishauri
vyama vinavyounda Ukawa kuwaelimisha wananchi ambao wanaamini kwamba siku ya
kupiga kura, watachagua Ukawa chama ambacho hakipo.
Wananchi
Wananchi
waliozungumza na Mwananchi walisema wanashangazwa na matokeo ya utafiti huo,
unaoonyesha hakuna mchuano mkali baina ya wagombea wa nafasi ya urasi tofauti
na hali ilivyo.
Julian
Mgigo, mkazi wa Buguruni alisema utafiti huo umefanywa baada ya waliohojiwa
kupatiwa simu na chaja, hivyo huenda matokeo hayo yasionyeshe uhalisia wa
mwenendo wa wagombea.
“Kwa
maoni yangu naona hilo linaweza kuathiri matokeo halisi ya kukubalika kwa
mgombea,” alisema.
0 comments:
Post a Comment