Tuesday, 8 September 2015

KATIBU WA CCM MKOA WA IRINGA AMTAMBULISHA MKEWE KUZIMA VILIMILIMI VYA WAPINZANI WAKE

KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Hassan Mtenga amemtambulisha mke wake hadharani akilenga kuumaliza uvumi uliokuwa unaenezwa na wapinzani wake wa kisiasa mjini Iringa kwamba ni muhuni asiye na mke.

Huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za ubunge wa jimbo la Iringa Mjini, Mtenga alisema “kwa muda mrefu kumekuwepo na wanasiasa uchwara wanaomtusi kwamba yeye ni muhuni asiye na mke.”

Huku akimkaribisha jukwaani mkewe huyo kwa jina la “Mama Zulfa” alisema waliocha kunadi sera zao na wakaingilia maisha yake binafsi sasa wanazidi kuumbuka.

“Naomba Mama Zulfa uwasilimie wapiga kura wa jimbo la Iringa Mjini,” alisema huku akimpa kipaza sauti.

“Kidumu Chama cha Mapinduzi, CCM oyee, Magufuli oyee, Mwakalebela Oyee, wangapi wataipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu ujao?” aliuliza huku sehemu kubwa ya wananchi hao wakishangilia na kunyosha mikono yao juu.

Mbali na wasanii mbalimbali wa Bongo Movies walioshiriki uzinduzi huo kutambulishwa, Mtenga alitumia fursa hiyo pia kumtambulisha upya, msaanii Jacob Steven (JB).

JB alisema alijiunga na CCM miaka 20 iliyopita baada ya kukutana na Mtenga na kumshawishi kuingia katika siasa.

“Watu wanaweza kujiuliza sana maswali kwanini mimi ni mwana CCM, basi sababu ndiyo hiyo na nawaomba kwa kumpa heshima mtu aliyenishawishi kujiunga na CCM mchagueni Mwakalebela awe mbunge wa jimbo lenu la Iringa mjini,” alisema.

Akijinadi, Mwakalebela mwenyewe alisema baada kuongozwa na mbunge kutoka upinzani kwa miaka mitano iliyopita, anataka kuona CCM mpya inazaliwa katika jimbo la Iringa ili ishiriki kikamilifu kumaliza kiu ya maendeleo wanaliyonayo wananchi wake.

Alisema anafahamu afanye nini kwa vijana, wafanyabiashara, akinamama, wakulima, wafugaji, makundi maalumu wakiwemo walemavu, walimu, wanamichezo na kwa wafanyakazi.

Alitaja vipaumbele vyake endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kuwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, maji, miundombinu, elimu na sekta michezo ambayo aliahidi kufanya kila atakaloweza ili timu ya Lipuli inayoshiriki ligi daraja la kwanza, ipande daraja.  

Akizungumzia changamoto ya vijana kukosa ajira, Mwakalebela alisema atatumia sehemu kubwa ya mshahara na marupuru yake kusaidia vijana bila kuangalia itikadi zao.

Mbali na bendi ya muziki ya Yamoto Bendi, wasanii wengine waliohudhuri uzinduzi huo ni pamoja na Blandina Chagula (Johari), Single Mtambalike (Richie), Dude na Irine Uyowa ambaye ni mmoja kati ya washindi sita wa ubunge wa viti maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

Reactions:

0 comments:

Post a Comment