Saturday, 26 September 2015

GARI LA KUBEBA WAGONJWA LALETA KIZAZAA JIMBO LA MUFINDI KUSINI


GARI la kubeba wagonjwa pamoja na wajawazito lililotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika kijiji cha Kasanga, kata ya Kasanga wilayani Mufindi mkoani Iringa zaidi ya miaka miwili iliyopita limechafua hali ya hewa.

Wananchi wa kijiji hicho, bila kuwataja majina, wamewalaumu watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kuchukua gari hilo kwa matumizi ya sehemu nyingine na wao kuletewa gari lingine bovu ambalo pia lilichukuliwa muda mfupi baadaye na kupelekwa Malangali.

Wakitaka gari hilo lirudishwe kijijini kwao mara moja, wananchi hao walimwambia mgombea ubunge wa jimbo la Mufindi Kusini kilipo kijiji hicho anayewania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mendrad Kigola kwamba hawatapiga kura, kama ombi lao hilo litapuuzwa.

Akizungumza kwa jazba mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Henry Saligo alisema; “Waziri Mkuu Mizengo Pinda hakukukosea kutupa msaada wa ambulance hiyo kijijini kwetu, tunashangaa watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi wanapata wapi jeuri ya kubadili maamuzi ya Waziri Mkuu.”


Wakimuhakikishia kumpa kura kwa wingi, wananchi wa kijiji hicho walimtaka mgombea huyo wa ubunge kuahidi kulifanyia kazi suala hilo ili haki yao ya kuwa na gari hilo isipotee.


“Waziri Mkuu alisikia kilio chetu na hasa kero wanayopata wajawazito wanapotakiwa kusafirishwa kwa ajili ya kupata huduma zingine ambazo hazitolewi katika zahanati yetu, huduma hizo zinahusisha huduma za rufaa,” alisema Saligo.

Huku akishangiliwa na wananchi wengine waliohudhuria mkutano wa hadhara wa mgombea huyo, alisema kama ahadi haitaahidiwa kutekelezwa hawatapiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Salingo alisema wapo baadhi ya watendaji katika halmashauri hiyo ambao kwa makusudi kabisa wamekuwa wakishindwa kutekeleza majukumu yao au kuyafanya kwa upendeleo jambo linaloongoza chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao.
Akitoa mfano, Salingo alisema miezi sita iliyopita, serikali ilitoa Sh Milioni 20 kwa ajili ya kuingiza huduma ya maji katika zahanati hiyo, lakini mpaka sasa huduma hiyo haijafika.


Naye Elizabeth Ndimbo alimuomba mgombea huyo kuhakikisha anawashughulikia watendaji wabovu wa halmashauri hiyo endapo atachaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa mbunge wake.
 
Mgombea huyo, Mendrad Kigola aliwatoa hofu wapiga kura wake akiahidi kufuatilia sababu za halmashauri hiyo kuliondoa gari hilo kijijini hapo.


Alisema ana hakika serikali itakayoundwa na mgombea urais wa CCM Dk John Magufuli itakuwa madhubuti, inayojali watu na ambayo haitakuwa na mchezo na watendaji wazembe.

Ili Dk Magufuli aweze kuunda serikali hiyo, aliwataka wananchi wa kijiji hicho na jimbo lake kwa ujumla kuwachagua wagombea wa CCM kwa kura nyingi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment