Monday, 28 September 2015

DK MAGUFULI AMPA SHAVU MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA MAFINGA MJINI, NI COSATO CHUMI

Dk Magufuli akimnadi mgombea ubunge jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi
Chumi akipiga push up kumuonesha Dk Magufuli jinsi alivyo fit 

Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi, Jimson Mhagama
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameing’arisha nyota ya mgombea ubunge jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi akiahidi katika mkutano mkubwa ambao haujawahi kutokea mjini hapo, kumfungulia milango ya Ikulu wakati wowote atakapotaka kuonana naye.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye uwanja wa Wambi mjini humo kwa uratibu wa Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi, Jimson Mhagama, Dk Magufuli alisema “Mafinga mmefunika” na akauliza kama mikutano ya wapinzani ilipata watu kama waliohudhuria mkutano huo na kujibiwa kwa sauti ya juu hapana.

Awali mkutano huo ulikuwa ufanyike katika uwanja uliozoeleka mjini Mafinga wa Mashujaa, kabla Mhagama na viongozi wenzake hawajauhamishia katika uwanja wa Wambi ili kukidhi mafuriko ya watu waliotarajia kujitokeza kumsikiliza Dk Magufuli na timu yake ya kampeni.

 “Chumi amefanya kazi serikalini; ni kijana mwenye uzoefu mkubwa sana serikalini. Najua mlimuhitaji siku nyingi na sasa amerudi ili aweze kuwatumikia,” Dk Magufuli alisema wakati akimwagia sifa mgombea huyo.

Chumi, msomi mwenye shahada ya uzamili katika masuala ya uhusiano wa kimataifa na mwenye shahada ya sayansi ya siasa na utawala alikuwa Afisa wa Kitengo cha Itifiki katika wizara ya Mambo ya Nje kwa miaka nane kabla hajaingia katika kinyang’anyiro hicho cha ubunge.

Huku wananchi waliofurika katika uwanja huo wakishangilia, Dk Magufuli aliendelea kumsifu Chumi akisema sifa yake nyingine ni kwamba wanafanana kwa kiasi fulani maumbo na sura zao na akawataka watakaoshindwa kumuita Chumi, wamuite Uchumi kwani ana hakika atafanya makubwa katika jimbo hilo na kwa maendeleo ya Taifa.

Kabla ya kumwagiwa sifa hizo, Chumi alimueleza mgombea huyo matatizo ya jimbo lake la Mafinga na kumuomba amsaidie kuyatatua mara tu atakapochaguliwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Akizitaja kero za jimbo hilo, Chumi alisema sehemu ya watu wake hawajafikiwa na huduma ya maji safi na salama huku hospitali ya wilaya hiyo ikihitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa na kuboresha huduma zake.

Aliomba pia huduma ya umeme ifikishwe katika vijiji visivyo na huduma hiyo jimboni humo pamoja na kuboresha barabara za mji huo ni pamoja na kujenga kilomita kumi kati yake kwa kiwango cha lami.

Kuhusu sekta ya Kilimo Chumi alisema, imeendelea kutokuwa na tija kwa wakulima wengi kwasababu ya ukosefu au ucheleweshaji wa pembejeo.

Akizungumzia jinsi msitu wa taifa wa Saohill unavyoweza kuchochea maendeleo ya watu wa jimbo hilo na wilaya nzima ya Mufindi, aliomba serikali ya Magufuli ianzishe utaratibu utakaowawezesha wananchi wa wilaya hiyo kupata asilimia 40 ya vitalu vinavyotolewa kila mwaka kwa ajili ya uvunaji.

Akijibu maombi hayo, Dk Magufuli aliwaomba wananchi wa wilaya hiyo kumchagua kwa kura nyingi yeye pamoja na wagombea ubunge na udiwani wa majimbo hayo ya Mafinga Mjini, Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini.

Wakati jimbo la Mufindi Kusini linawania kwa mara nyingine tena na Mendrad Kigola aliyekuwa mbunge wake kwa miaka mitano iliyopita, la Mufindi Kaskazini linawania kwa mara nyingine tena na Mahamudu Mgimbwa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Katika tukio lingine, Dk Magufuli aliwaamuru wagombea hao kupiga push up baada ya wananchi waliokuwa wakimsikiliza kumuomba afanya hivyo muda mfupi mara baada ya kumaliza hotuba yake.

“Leo sipigi mimi, kwa niaba yangu nawataka wagombea ubunge wote wa jimbo hilo waje hapa na kufanya hivyo kwa niaba yangu,” alisema kabla Chumi, Mgimwa na Kigola hawajajitokeza kupiga push up huku wakishangiliwa.


Wakati wagombea wawili walimaliza zoezi hilo salama, hali haikuwa hivyo kwa Mgimwa kwani alitaka kudondokea pua baada ya kujaribu kupiga push up ya pili na kuacha kicheko kikubwa kwa wananchi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment