Sunday, 13 September 2015

COSATO CHUMI AANZA MCHAKAMCHAKA WA KUTWAA JIMBO LA MAFINGA MJINI, AMPONGEZA KIKWETE DHIDI YA LOWASSA

MGOMBEA ubunge jimbo la Mafinga Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Cosato Chumi juzi amezindua kampeni zake za kuwania kiti hicho akiwataka watanzania kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kumtosa aliyekuwa rafiki yake wa jirani, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.

Baada ya kutoswa na CCM, Lowassa alikimbilia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na akateuliwa kuwa mgombea wake urais ambaye pia anawakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kinyang’anyiro hicho.

Akimpigia debe mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, Katibu wa CCM wa wilaya ya Mufindi, Jimson Mhagama amemfananisha mgombea huyo wa Ukawa na nyuki wa mashineni ambao kwa kawaida huwa hawana uwezo wa kung’ata.

Chumi aliyesindikizwa na wagombea wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Mahamudu Mgimwa na Mufindi Kusini, Mendrad Kigola katika uzinduzi huo, alisema kama Rais Kikwete angekuwa hamfahamu vizuri Lowassa huenda angemuunga mkono katika mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM.

“Rais Kikwete aliamua kumtosa Lowassa kwasababu hakutaka kutuachia mtu mwenye matatizo na mpiga “deal”, kwahiyo kufahamiana naye kumekuwa na faida kubwa kwa watanzania,” Chumi alisema.

Akiomba kura kwa mamia ya wananchi waliofurika katika uzinduzi huo uliofanyika katika uwanja wa Mashuja mjini Mafinga, Chumi aliyeshika tochi kubwa muda wake wote aliokuwa akiongea, alisema anataka kuwa mbunge wa jimbo hilo ili akawamulike na kuwafichua wazembe wanaochelewesha au kuhujumu kwa makusudi huduma katika sekta mbalimbali jimboni humo.

Akitaja vipaumbele vyake endapo wananchi wa jimbo hilo watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao, alisema atahakikisha katika kipindi cha miaka mitano ijayo jimbo hilo linakuwa na huduma bora ya maji, afya, miundombinu na elimu.

Alizitaja sekta zingine atakazozitupia jicho kuwa ni pamoja na ya biashara na ulinzi na usalama kwa kuhamasisha ujenzi wa vituo vidogo vya Polisi katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Kwa upande wake, Mgimwa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii alisema; “Majimbo yote wilaya ya Mufindi yamepiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.”

“Tulikuwa hatuna lami mjini, leo tuna barabara zenye lami na tumeanza ujenzi wa barabara ya Mgololo kwa kiwango cha lami. Tumejenga kilomita tatu na tumepata fedha kwa ajili ya kujenga kilometa nane mwaka huu wa fedha,” alisema.

Katika sekta ya afya na fedha, alisema wodi ya kisasa ya wazazi imejengwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi ili kuboresha huduma kwa wajawazito huku huduma za benki zkiongezeka kutoka benki moja hadi tatu, ambazo ni Mucoba, NMB na Crdb.

Wengine waliohudhuria kampeni hizo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu aliyezungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mahamudu Madenge aliyeponda kipaumbele cha Lowassa, cha elimu, kwamba kinamsuta jimboni kwake Monduli.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment