Saturday, 26 September 2015

CCM, ACT WAZALENDO WAMKOMALIA MCHUNGAJI MSIGWA


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo vinaongeza kasi ya kuwashawishi wapiga kura wa Jimbo la Iringa Mjini kutomchagua kwa awamu nyingine tena mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Mchungaji Msigwa alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tofauti ya kura 828 baada ya kupata kura 17,744 dhidi ya kura 16,916 alizopata mgombea wa CCM, Monica Mbega.

Katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea jimboni humo, mgombea ubunge kupitia ACT Wazalendo, Chiku Abwao amemtuhumu Mchungaji Msigwa kutumia vibaya fedha za mfuko wa jimbo na kuwaomba wapiga kura wamnyime kura katika uchaguzi wa mwaka huu.

Abwao aliyekuwa mbunge wa viti maalumu mkoa wa Iringa kupitia Chadema, alisema katika mkutano wake wa kata ya Kihesa kwamba; “miaka mitano ya ubunge wa Mchungaji Msigwa ilikuwa ni miaka iliyorudisha maendeleo ya wananchi wa jimbo la Iringa Mjini kwasababu ya ubinafsi wa Mchungaji Msigwa.”

Alisema wananchi wa jimbo hilo wakiamua kuulingnanisha utendaji kazi kati ya Mchungaji Msigwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kabla yake Monica Mbega; kwa vyovyote vile Mbega anamzidi kwa mbali Mchungaji Msigwa kwa kusaidia maendeleo ya wananchi.

Aliwataka wamchangue kuwa mbunge wa jimbo hilo, Abwao alisema ataitumia miaka mitano ijayo kumfanya awe mbunge wa mfano wa kuigwa katika kuzishughulikia kero na kupigania maendeleo ya wananchi.
 
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga amewataka wapiga kura wa jimbo la Iringa Mjini kutomchagua Mchungaji Msigwa kwani hana rekodi inayompa kibali cha kuwa mwakilishi wa wananchi kwa mara nyingine.


“Msigwa katika maisha yake ya ubunge, amekuwa mbunge wa maandamano, mambo ya kitaifa na wa kulalamika. Akasahau kushghulikia kero za watu wa Iringa na leo anataka tena huruma yenu,” alisema.

Mtenga alisema mbali na kushindwa kuhudhuria vikao vya barala la madiwani Iringa Mjini ambavyo moja ya majukumu yake ni kupanga mipango ya maendeleo ya jimbo, Mchungaji Msigwa alikuwa akipinga bajeti zote akiwa bungeni.

“Pamoja na kupinga, serikali iliendelea kutekeleza mipango yake kwa kupitia Ilani ya CCM na mambo mengi yaliyofanywa katika kipindi cha ubunge wake, yamefanywa kwasababu serikali ya CCM inawapenda watu wa Iringa hivyo huu ni wakati muafaka wa kuichagua kwa nafasi zote ili ikasimamie maendeleo yetu kwa kasi kubwa zaidi,” alisema.

Katika  mkutano uliofanyika kata ya Kihesa hivikaribuni, Mtenga aliwataka wana Iringa kuachana na siasa za mihemumko  ya kupigana na kuzomeana katika mikutano ya kampeni bali wafanye siasa za kistaarabu na kwani kuna maisha mengine  nje ya siasa.

Mtenga aliitupia lawama Chadema akisema imeleta vijana wapatao 48 kutoka jijini Arusha kwa ajili ya kuanzisha mijadala mbalimbali kwenye vituo vya mabasi na vya magazeti inayolenga kuwabeza wanaoishabikia CCM.


Katika mikutano yake mbalimbali, Mchungaji Msigwa ameitetea rekodi yake ya utendaji akiwa mbunge wa jimbo kwa miaka mitano akisema haiwezi kulinganishwa na wabunge waliopita.

Mchungaji Msigwa alisema jimbo la Iringa Mjini limepiga maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali za kijamii tofauti na ilivyokuwa wakati lililipokuwa likiongozwa na wabunge wa CCM.

Alisema katika kampeni zake za mwaka 2010 aliwaambia wananchi wa jimbo hilo kwamba moja ya kazi kubwa atakayoifanya ni kuhakikisha wanazitambua na kuzidai haki zao pale zinapopokonywa na walioko madarakani.

“Watu wa Iringa Mjini sasa wanajivuna kwasababu wanajitambua na wajua maendeleo yanatakiwa kuletwa na serikali yao iliyopo madarakani, wanajua kwamba serikali hiyo imeshindwa na sasa wanapaza sauti zao ili ije serikali ya Ukawa,” alisema.

Aliwataka wana Iringa kumchagua Mgombea urais wa Ukawa , Edward Lowassa, yeye kuwa mbunge wa jimbo hilo na madiwani wote ili walete mabadiliko ya kweli.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment