Friday, 7 August 2015

ZITTO KABWE KUHUTUBIA IRINGA JUMAPILI, KUMTAMBULISHA CHIKU ABWAO MGOMBEA UBUNGE IRINGA MJINI


ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chiku Abwao ameshinda kura za maoni za chama cha ACT Wazalendo ikiwa ni siku chache toka ajiunge na chama hicho.

Ushindi mwembamba wa kura 23 alizopata dhidi ya mgombea mwenzake Daudi Masasi aliyepata kura 21, umemuweka katika nafasi ya kuteuliwa na chama chake hicho kipya kuwania ubunge wa jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

Kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo, Abwao alipania kugombea ubunge katika jimbo la Isimani kupitia Chadema, lakini kwa kile alichoita hila zilizokuwa zikifanywa dhidi yake na mbunge wa jimbo la Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa ndoto yake hiyo imekoma.

“Sina mahusiano mazuri ya kisiasa na Mchungaji Msigwa, amekuwa adui yangu mkubwa kisiasa mara baada ya kupata ubunge Iringa Mjini; nilikuwa sipati fursa nzuri ya kutekeleza majukumu yangu ya kibunge mjini Iringa kwasababu kila nililokuwa nikifanya alilitafsiri kwamba linalenga kumdhohofisha kisiasa,” alisema.

Alisema ili kuepukana na fikra hizo za Mchungaji Msigwa aliamua kujijenga kisiasa katika jimbo la Isimani ambako nako alipelekewa wapinzani ili aifurukute.

“Hayo na mengine mengi ndani ya Chadema yamenifanya nitafakari na baadaye kuamua kujiunga na ACT Wazalendo,” alisema.

Kabla ya kushinda kura hizo za maoni Abwao alisema Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anatarajia kuja mjini Iringa Jumapili Agosti 9 kwa lengo la kumtambulisha rasmi kwa wakazi wa mjini Iringa.

Alisema Kabwe atakayeambatana na aliyekuwa Mbunge wa Kasulu, Moses Machali na Afande Sele na viongozi wengine wa ACT atafanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Mwembetogwa jumapili hiyo.

“Naomba wana Iringa wajitokeze kwa wingi ili waje kusikiliza sera za ACT Wazalendo wakati nikitambulishwa,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment