Thursday, 6 August 2015

TANAPA WAJA NA ZAWADI LUKUKI KWA WATAKAOTEMBELEA HIFADHI ZA TAIFA, WASAFIRISHA WATALII WAPUNGUZA BEI


KAMPUNI ya kuongoza watalii ya Tatanca Safari and Tours ltd ya mjini Iringa imeatangaza ofa itakayowawezesha makundi tofauti ya wakazi wa mikoa ya nyanda za juu kutembelea hifadhi za Taifa kwa gharama nafuu.

Hifadhi hizo ni pamoja na hifadhi ya Ruaha, Mikumi, Udzungwa na Kitulo ambazo zote zipo jirani na Iringa, na Katavi iliyopo mkoani Katavi.

Afisa Utalii wa Nyanda za Juu Kusini wa wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Risala Kabongo alitaja vivutio mbalimabli vilivyopo katika hifadhi hizo kuwa ni pamoja na wanyamapori waishio nchi kavu na majini, maua na mimea mingine ya kuvutia, mito, maporomoko ya maji na mandhari ya kuvutia ya miamba, milima na mabonde

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Denis Ngede alisema ofa hiyo inalenga kuitia wito wa kuhamasisha watanzania kutembelea hifadhi za Taifa kupitia kampeni yake ya miezi sita ya ‘Tembelea Hifadhi Ufaidike’.

Ngede alisema kwa kutumia magari yao yenye uwezo wa kubeba watu nane hadi 35, mtanzania anapewa ofa ya kutembelea hifadhi hizo kwa kiasi kinachoanzia Sh 30,000.

 “Kwahiyo tupo tayari kusafarisha makundi ya watu nane hadi 35 kwa gharama hiyo tu kwa hifadhi ya jirani zaidi kama Ruaha na kutakuwepo na nyongeza ya kiasi kidogo cha fedha kwa hifadhi zilizopo mbali zaidi kama ile ya Kitulo na Katavi,” alisema.

Mbali na kampuni hiyo, Afisa Utalii wa Nyanda za Juu Kusini wa Bodi ya Utalii Tanzania, Gervas Mwashimaha alizitaja kampuni zingine za mjini Iringa zinazoweza kutoa ofa inayofanana na hiyo kuwa ni pamoja na Masoko Tours, Iringa Safari Tours na Warthog.

Akizungumzia kampeni hiyo, Kaimu Meneja Masoko wa Tanapa, Victor Ketansi alisema; “kampeni hii itakuwa ya miezi sita, imeanza Julai 1 na itaisha Desemba mwa huu.”

Alisema watanzania wanaotaka kutembelea hifadhi hizo wanaweza kujiandikisha na kulipia katika vituo vyao (ofisi) vilivyopo mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Iringa, Morogoro na Mbeya.

Alisema watanzania watakaotembelea hifadhi hizo watajipatia zawadi mbalimbali ambazo kwa mujibu wa Catherine Mbena wa Tanapa ni pamoja na kupewa ofa ya kutalii katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti au Gombe na kulala katika hoteli yenye hadhi ya nyota tano kwa siku tatu endapo utatembelea hifadhi yoyote ile nchini zaidi ya mara nne katika kipindi hicho cha kampeni.

Katika kipindi hicho cha kampeni hiyo, Ketansi alisema TANAPA kwa kushirikiana na wadau wake inalenga kuhamasisha watalii wa ndani zaidi ya 500,000 watembelee hifadhi hizo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment