Thursday, 27 August 2015

SERIKALI YATOA MASHARTI KWA VYAMA VINAVYOTAKA KUTUMIA HELIKOPTA KATIKA KAMPENI ZAKE


Serikali kupitia mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania  imeatangaza kupiga marufuku  matumizi ya Helikopta katika kampeni za wanasiasa katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Tangazo lilitolewa na Charles M. Chacha Kaimu mkurugenzi mkuu mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania limebainisha kuwa  Mamlaka hiyo imepiga marufuku matumizi hayo baada ya  kugundua kwamba kumekuwa na matumizi mabaya ya huduma hizi kinyume na kanuni za usafiri wa anga nchini na weledi unaozingatia taratibu za kitaaalamu na miongozo katika usafiri wa anga.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa  Mamlaka inatambua kwamba matumizi ya helikopta wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 yanatarajiwa kuongezeka na kuna uwezekano wa kuleta athari za kiusalama kwa maisha ya watu na mali pamoja na watumiaji.

Tangazo hili linatolewa kwa mamlaka aliyopewa Mkurugenzi Mkuu chini ya Sheria Namba 80 ya Usafiri wa Anga na kanuni zake zinazohusiana na masuala ya usafiri wa anga nchini zilizowekwa kwa lengo, hususan, kuhakikisha usalama katika matumizi ya vyombo vya usafiri wa anga sambamba na kulinda usalama wa umma na mali wakati wa matumizi ya vyombo husika.

Watoa huduma za usafiri wa helikopta au ndege na marubani wake wanaokodishwa kutoa huduma wakati wa kampeni, na mtu yeyote anayetarajiwa kutumia huduma hiyo wanakumbushwa kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafiri wa anga na ikibidi kuomba kibali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania.

Aidha, Helikopta yeyote itakayotoa huduma katika kampeni za kisiasa lazima iwe ina cheti halisi cha usalama wa kuruka kilichotolewa na mamlaka husika ya helikopta ilikosajiliwa. Kwa hapa nchini cheti hicho ni lazima kiwe kimetolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga.

Endapo helikopta itakuwa ina usajili wa nje ya Tanzania, mtu anayetarajia kuitumia hapa nchini ni lazima apate kibali cha kuiingiza nchini na kuitumia kwa usajili wa nchi iliyotoka kama ilivyoainishwa katika Waraka wa Mamlaka unaoainisha taarifa za usafiri wa anga

Mamlaka hiyo Imewataka watumiaji  kuhakikisha wanapoomba kibali wawe wamekidhi vigezo vya waraka huu ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nakala za nyaraka zinazopaswa kuwasilishwa zikiwemo cheti cha usajili wa ndege, cheti cha ndege kwa usalama wa kuruka, cheti cha leseni za radio za ndege, cheti cha bima, makubaliano/mkataba wa kukodisha ndege hiyo, utaratibu wa kufanya matengenezo ya ndege hiyo, leseni za marubani, na ushahidi wa karibuni wa matengenezo ya ndege hiyo.

Katika hatua nyingine  taarifa hiyo imesema Rubani Mkuu anawajibika kuhakikisha kwamba vituo vya Mamlaka vya kuongoza ndege vinavyohusika katika eneo atakalokuwepo au kwa utaratibu wa uongozaji ndege, wanakuwa na taarifa za mpango wake mzima wa safari husika kwa siku au wakati husika.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment