Tuesday, 11 August 2015

PROFESA MSOLLA ASHINDA RUFAA YAKE, KURA ZA MAONI YA UBUNGE CCM KILOLO KURUDIWA KESHO


KESHO ndio kesho Agosti 12, pale macho na masikio ya wengi yatakapoelekezwa katika Jimbo la Kilolo, mkoani Iringa linalorudia kura za maoni ya ubunge zitakazompata mgombea atakayepeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kura hizo zinarudiwa baada ya Mbunge wa Kilolo anayemaliza muda wake, Profesa Peter Msolla kushinda rufaa iliyokuwa ikipinga matokeo yaliyompa ushindi Mkuu wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Venance Mwamoto.

Profesa Msolla alikata rufaa hiyo kwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kilolo na nakala ya rufani yake kuwasilishwa kwa Katibu wa CCM wa Mkoa na kwa uongozi wa chama hicho Taifa waliotoa maamuzi ya kubatilisha matokeo ya kua hizo baada ya kuridhishwa na maelezo ya rufani ya mbunge huyo.

Katika uchaguzi huo wa awali, uliopelekea pia kata tatu kati ya 24 za jimbo hilo kurudia uchaguzi wake kwa kile kilichoelezwa kulikuwepo na udanganyifu katika mchakato wake wa upigaji kura, Mwamoto alishinda kwa kupata kura 11,200 huku Profesa Msolla akiwa mshindi wa pili kwa kujipatia kura 10,014.

Kabla kata hizo tatu za Lugalo, Uhambingeto na Nyarumbu hazijarudia uchaguzi huo ulioshirikisha wagombea 15, Profesa Msolla alikuwa akiongoza kwa kura 13,409 dhidi ya kura 9,749 alizopata Mwamotto.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kilolo, Clement Mponzi alisema uchaguzi huo unarudiwa kesho Agosti 12 katika kata zote ili ili kumaliza utata uliothibitishwa katika malalamiko yaliyotolewa kupitia rufani ya Profesa Msolla.

Mponzi alisema utaratibu wa upigaji kura utaanza saa 2.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni katika vituo vile vile vya awali na akawataka wana CCM wote wenye sifa kujitokeza kushiriki marudio ya uchaguzi huo.

Aliwataka pia wagombea kuwahimiza mawakala wao kufika mapema katika vituo vya kupigia kura na kuzingatia taratibu zote ikiwemo ya kuhakiki wapiga kura wanaostahili ili kuepuka lawama zisizo na msingi.

Kwa kupitia rufaa yake hiyo, Profesa Msolla alisema anapinga matokeo hayo kwasababu yalitangazwa bila kuridhiwa na wagombea au mawakala wao pamoja na kwamba alikuwa anaongoza kwa kura 13,409.

Alisema kura zake ziliyoyoma baada ya Katibu wa wilaya bila kushirikisha kamati ya siasa ya wilaya hiyo kuamuru kata hizo kurudia uchaguzi kwa madai kwamba wasimamizi wa uchaguzi wa kata hizo walichelewa kuwasilisha matokeo yake ndani ya muda uliopangwa.

“Na kimsingi kata zilizoamuriwa zirudie uchaguzi kwa kisingizio kwamba matokeo yake yalichelewa wakati kuna kata nyingine nyingi tu nazo zilichelewesha matokeo yake ni baadhi ya kata ambazo mimi nilipata kura nyingi zaidi ikilinganishwa na wagombea wengine,” alisema.

Alisema pamoja na kata hizo kuamriwa zirudie uchaguzi huo bila kufuata taratibu, vifaa vya kupigia kura vilifkishwa vituoni kwa kuchelewa na viliondolewa katika baadhi ya vituo hivyo kabla ya muda unaotakiwa.

Alisema pamoja na kata hizo kurudia uchaguzi huo, uhesabuji wa matokeo ya jumla ya jimbo hilo uligubikwa na udanganyifu mkubwa kwani baadhi ya vituo alivyoongoza kwa kura; kura hizo hazikuwepo tena.

Akizungumzia dosari iliyopelekea uchaguzi katika jimbo hilo kurudiwa, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema kuwa kuna baadhi ya wagombea hawakuridhika na matokeo hivyo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama hicho wameamuru uchaguzi huo kurudiwa ili kila mmoja kupata haki yake anayostahili.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment