Monday, 10 August 2015

MUFINDI YAANZA KUZALISHA VIAZI LISHE VYENYE VITAMIN A KWA WINGIWILAYA ya Mufindi ni moja kati ya wilaya saba nchini zitakazoanza kuzalisha viazi lishe vyenye asilimia kubwa ya vitamin A ikilinganishwa na aina nyingine ya vyakula vya mbogamboga, matunda na mizizi.

Mbali na Mufindi, wilaya zingine zilizoingizwa katika mpango huo na shirika la kimataifa linaloshughulikia mazao ya viazi (CIP) ni pamoja na Iringa, Ulanga, Mbozi, Chunya, Gairo na Wanging’ombe.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Ndimmyake Mwakapiso alisema viazi hivyo ni aina ya viazi vitamu vyenye rangi ya chungwa.

Alisema viazi hivyo vina asilimia 90 ya vitamini “A” inavyohitajika katika mwili wa binadamu ili kumuwezesha kuwa na uwezo mzuri wa kuona, kujenga ubongo wa watoto chini ya miaka mitano na kuimarisha afya ya wajawazito.

Alisema, mradi huo umeanza kutekelezwa kupitia vikundi vya wakulima vinavyootoesha mbegu kwenye maeneo yenye miundombinu ya umwagiliaji.

Maeneo hayo yapo katika viijiji vya Igomaaa na Lugolofu pamoja bustani ambazo hutambulika kwa jina la vinyungu zilizopo kwenye vijiji vya Lugema, Mabaoni na Makungu.

Mwakapiso alisema mbegu zitakazozalishwa zitagawiwa kwenye vijiji 18 ambayo vimechaguliwa kuanza kutekeleza mradi huo baada ya msimu wa mvua kuanza.

 “Vijiji vitakavyo pata mbegu hizo ni Makungu, Mabaoni, Lugema, lugolofu,  Iramba, Ikimilinzowo, Nyigo, Nyanyembe, Maguvani, Idetero, Mkangwe, Ikangawani na Idumulavani,   Igomaa, Utosi, Kibada, Ugenza na Ikweha”, alisema.

Alisema viazi vikizalishwa kwa wingi na kuongezwa thamani ya zao hilo vitamwongezea mkulima kipato kwani soko lake linapatikana kwa urahisi huku vikiwa na uwezo wa kuzindikwa kwa kutengeneza Kripsi, Mikate, Chapati, Biskuti, juisi na Unga wa lishe.

Aliwataka wakulima watakaopata mbegu hizo wazitumie vizuri ili uzalishaji wa zao hilo ulete matokeo yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi na hatimaye kuwaondoa katika umasikini.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment