Monday, 31 August 2015

MSAFARA WA LOWASSA WAPUUZA OMBI LA MCHUNGAJI MSIGWA KUSUSIA BIASHARA ZA ASAS
MAGARI yaliyopo katika msafara wa mgombea urasi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa yamejaza mafuta katika kituo cha mafuta cha kampuni ya ASAS cha mjini Iringa ikiwa ni siku moja baada ya mgombea ubunge Jimbo la Iringa kupitia chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa kuwataka wafuasi wa chama hicho kususia biashara za kampuni hiyo.

Magari hayo ni pamoja na gari linalotumiwa na mgombea huyo na Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye yenye namba T841 CYP na T802 DCM.

Pamoja na magari hayo, mengine yaliyojaza mafuta katika kituo cha kampuni hiyo cha Iringa Filling Station cha mjini Iringa mapema jana ni pamoja na lenye namba T148 BLE, T 739 CDT na basi dogo aina ya Coaster linalotumiwa na wanahabari walioko katika msafara wa mgombea huyo.

Akihutubia umati mkubwa wa wakazi wa mjini Iringa na vitongoji vyake juzi, Mchungaji Msigwa alisema kuna mfanyabiashara mkubwa wa mjini Iringa anazuia vijana kushiriki katika harakati za mabadiliko.

“Juzi nilimpigia simu, nikamwambia asitumie biashara zake kufanya siasa za aina hiyo. Nawaomba wananchi mnaounga mkono mabadiliko msimpe adhabu nyingine yoyote, mpeni adhabu moja kubwa ya kutonunua bidhaa zake,” alisema bila kumtaja mfanyabiashara huyo japokuwa baadhi ya wananchi walikuwa wakimtaja kwa sauti “ASAS”.

Mchungaji Msigwa aliwaomba wananchi hao kutojaza mafuta katika vituo vyake vya mafuta lakini pia kususia bidhaa zingine zinazozalishwa na kampuni hiyo.

Mbali na kampuni hiyo kujishughulisha na biashara ya mafuta ya mitambo na magari, inafanya pia biashara ya usafirishaji, majengo ya kupangisha na maziwa.

Lowassa
Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa amesema kama Watanzania watashindwa kufanya mabadiliko kwa kupiga kura kuing’oa CCM madarakani mwaka huu, hawataweza kufanya hivyo tena, huku akihoji kama vyama tawala mbalimbali katika nchi za bara la Afrika vimeng’oka madarakani: “Kwa nini isiwe CCM”.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni katika Uwanja wa Gangilonga mjini Iringa, Lowassa aliyeambatana na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye alisema vyama tawala vilivyokuwa rafiki na CCM vimeshang’oka madarakani na kwamba hivi sasa ni zamu ya chama hicho tawala kuondolewa.

 “Nataka kura nyingi ili hata wakiiba tushinde, asilimia 90 ziwe zetu hizo 10 waache waibe. Msipoiondoa CCM mwaka huu hatutaiondoa tena, CCM na Tanu walikuwa na marafiki zao lakini karibu wote wameondoka,” alisema.

Alivitaja vyama hivyo kuwa ni Chama cha Kanu cha nchini Kenya, Malawi Congress Party cha Malawi na UNIP cha Zambia.

 Katika mkutano huo, Lowassa alirudia vipaumbele vya ilani ya uchaguzi ya Ukawa, huku akimponda mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CCM, Frederick Mwakalebela kuwa hawezi kushinda kwa maelezo kuwa amepanda gari bovu.

“Namfahamu Mwakalebela, ni kijana mzuri lakini amepanda gari bovu, na bahati mbaya aliyonayo hata kama angekuja huku hawezi kumfikia Mchungaji Msigwa,” alisema.

Tofauti na matukio mengine ya mgombea huyo, katika mkutano huo wa Iringa alitumia dakika 25 kuhutubia mkutano huo, baada ya kuanza saa 11.33 jioni na kumaliza saa 11.58.

Baada ya kumalizika kwa mkutano huoi, baadhi ya wananchi walilisukuma gari la Lowassa na mgombea ubunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema, Mchungaji Peter Msigwa hadi katikati ya mji huo kabla ya magari hayo kushika kasi na kuwaacha wakiendelea kukimbia barabarani huku wakiimba nyimbo mbalimbali.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment