Monday, 10 August 2015

CCM NI HODARI WA KUIBA KURA?


Mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward Lowassa ameituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura hivyo akawataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili hata sehemu ya kura hizo ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa kishindo.

Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani aliuambia umati wa wafuasi wa Ukawa uliojitokeza jana kumpokea katika ofisi za makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni kuwa ili kufanikisha ushindi wa kuwawezesha kuingia ikulu hawana budi kushikamana, kushawishiana kupiga kura kwa wingi na kuzilinda Oktoba 25.

Kauli hiyo ya Lowassa ambaye amelelewa kisiasa na CCM tangu alipojiunga akiwa mdogo mwaka 1977, inaendeleza tuhuma ambazo hutolewa na vyama vya upinzani kuwa chama hicho huchakachua matokeo wakati wa uchaguzi.

Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani.

“Tukiwa na umoja, tukiwa na mshikamano tutawaondoa Jumapili asubuhi sana. Tutahitaji mshikamano, tatahitaji ushawishi wa kupiga kura tupate angalau asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tuwasamehe,” alisema Lowassa katika hotuba yake iliyokuwa inakatishwa na kushangiliwa na na salamu ya CUF ya “Hakiii” na kujibiwa “kwa wote.”

“Hodari sana wa kuiba CCM kura. Sasa tupate kura nyingi za kutosha hata wakiiba kura hausikii na kuna usemi wa Chadema unaosema ‘piga kura, linda kura’ na sisi CUF ni hodari sana wa mambo hayo.”

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kwa simu kuhusu madai hayo, alijibu kwa ujumbe wa maneno kuwa asingeweza kuzungumza bali atumiwe ujumbe, na alipotumiwa ujumbe huo hakujibu.

Lubuva: Aeleze wanaibaje

Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)  Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba kura.

“Ili kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti wa kutosha juu ya tuhuma hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba, vinginevyo nitaeleza kitu ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu aliyekuwa serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi, angeeleza.”

Tume huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu na sheria na iwapo kuna mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga ili ofisi yake ifanye utafiti wa kina.

“Naomba nieleweshwe kura huwa zinaibiwa vipi? Hii imekuwa ni hisia, wengine wanasema tutaibiwa kura zetu wakati upande mwingine unasema hawa wataleta fujo kwa visingizio vya kuibiwa kura,” alisema Jaji Lubuva.

Lowassa ambaye alihamia Chadema siku 11 zilizopita na baadaye kuteuliwa kugombea urais kwa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, alisema safari ya Ikulu itafanikishwa kwa kupiga kura na siyo maandamano, hivyo Watanzania watunze shahada za kupigia kura. Hata hivyo, hakuendelea kueleza undani kuthibitisha ni namna gani CCM huiba kura.

Kiongozi huyo aliyeonekana mwenye furaha, aliwataka wanawake nao kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji wa kura huku wakiwa wameshapika vyakula majumbani mwao ili nao wapate fursa za kupiga na kulinda kura.

Lowassa alisema ameingia Ukawa ili kuandika historia ya nchi kukuza uchumi na kuondoa umaskini na kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya “mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya CCM.”

Ukawa kutoyumba

Mbunge huyo wa Monduli anayemaliza muda wake, alisema Ukawa ipo imara haitayumbishwa kirahisi na wafitini, licha ya baadhi ya watu kujipitisha kwa viongozi wa juu na kutaka kuwarubuni ili umoja huo utetereke.

“Wanakuja kupitisha hela na kuhongahonga lakini viongozi wapo imara…hawahongeki hawa! Wanapita na maneno kwenye magazeti ya ufukuzi ufukuzi, nawaambia muwapuuze,” alisema Lowassa bila kuwataja wahusika.

Alisema kuna baadhi ya watu wanaleta propaganda kuwa Ukawa ikiingia madarakani nchi haitatawalika kiasi cha kuwatisha wafanyabiashara kukimbiza fedha zao nje ya nchi, jambo ambalo si la kweli.

“Waongo wakubwa hao…nchi itatawalika kuliko awali, Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuli, wasiwadanganye mkimbize hela zenu..tupo imara,” alisema.

MWANANCHI

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kina wagombea wawili wanaowania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Madai hayo mapya ya Profesa Lipumba yametolewa siku tatu baada ya kujiuzulu uenyekiti CUF, akisema hiyo ni moja ya sababu za kuachia nafasi yake kutokana na uamuzi uliofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuhusu mgombea urais.

Akizungumza wakati akitangaza kujiuzulu wiki iliyopita, Profesa Lipumba alisema dhamira yake ilikuwa inamsuta kwa kuwaingiza ndani ya Ukawa watu kutoka CCM, waliokuwa wanapingana na maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na kuwapa fursa ya kuwania urais.

Juzi usiku katika mahojiano aliyoyafanya na Azam TV kutoka Kigali alikosema anafanya utafiti, Profesa Lipumba alisema kumpa nafasi waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema ndani ya Ukawa, ni sawa na CCM kusimamisha wagombea wawili (Lowassa) na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.

Katika mahojiano hayo ya simu, Profesa Lipumba ambaye wiki mbili zilizopita alimpokea Lowassa akisema ni mtu safi na kwamba, ufisadi ndani ya CCM ni mfumo  alisema katika kujiuzulu kwake hakutumiwa na CCM kuparaganyisha Ukawa, bali walikuwa tayari wameparaganyika.

“Ukweli ni kwamba tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa tulikuwa na wagombea watatu… mimi, Dk Willibrod Slaa, (Katibu Mkuu wa Chadema) pamoja na Dk George Kahangwa (NCCR-Mageuzi) ambaye alikiri kuwapo makubaliano hayo.

“Tulikutana nyumbani kwangu tukakubaliana Dk Slaa apeperushe bendera ya Ukawa, lakini tumewekwa kando,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema yupo Rwanda kwa muda na anafanya utafiti kuona namna gani Tanzania inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa kiuchumi.

Pia alisisitiza kuwa hajahama nchi na kwamba wiki hii anatarajia kurejea nchini.

Agosti 6, mwaka huu Profesa Lipumba alijivua  uenyekiti wa CUF wakati mkakati wa vyama vya upinzani kushirikiana kushika dola ukiwa umeshika kasi.

MTANZANIA

WAZIRI Mkuu wa zamani ambaye pia ni mgombea urais kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka wananchi kuhamasishana na kumpigia kura ili apate ushindi wa asilimia 90.

Alisema akipata ushindi huo na hata kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiiba asilimia 10 ya kura zake, bado Ukawa watabaki na asilimia 80 ambao ni ushindi mzuri.

Akizungumza na wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni, Dar es Salaam jana, Lowassa alisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuishinda CCM.

“Hawa jamaa ni hodari sana wa kuiba kura, tunahitaji kufanyika kwa ushawishi na mshikamano, kila mtu anahitaji kushawishi wenzake angalau watano ili tujihakikishie ushindi wa asilimia 90 pindi watakapoiba asilimia 10 tutaibuka na ushindi wa asilimia 80.

“Ni bora tuhakikishe tunapata kura nyingi ili wakiiba wasiweze kutufikia na jambo jingine tulinde kura zetu kama ambavyo sasa Chadema wanafanya na CUF, wamekuwa ni bingwa wa kazi hiyo kwa muda,” alisema.

Alisema kama watahakikisha hilo linafanyika na wanashikamana pamoja, itakuwa vigumu kwa CCM kuwashinda kirahisi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Lowassa aliwaambia jambo muhimu wanalotakiwa kutambua ni kutoyumba, kwani kwa kufanya hivyo watasababisha kujiwekea mazingira magumu kuingia Ikulu na pia watambue kuwa kura ndiyo itawawezesha na si njia ya maandamano hivyo aliwaomba kuhifadhi shahada zao.

“Hivi sasa Watanzania wapo makini na wapo tayari kuongozwa kwenda Ikulu Oktoba 25, jambo la msingi ni kuhakikishi mnalinda shahada zenu na kutumia nidhamu, tukitumia kura hawa tutawashinda Jumapili asubuhi, hawana hoja tena washachoka,” alisema na kuongeza:

“Jambo muhimu ni kutoyumba, tukiyumba Ikulu mjue hatuingii, huko tutaenda kwa kura na si kwa maandamano naomba sana mhifadhi shahada zenu.”

UCHUMI

Lowassa, alisema miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakimuumiza tangu akiwa CCM ni nchi kutosonga mbele kimaendeleo.

Alisema CCM imekuwa ikiendesha uchumi kwa tabu na adha, jambo ambalo lilifanya kuwauliza wananchi kwamba wakati Mkapa anaondoka madarakani dola ilikuwa shilingi ngapi na sasa ni ngapi? Wananchi wakajibu ilikuwa 1,000 na leo shilingi 2,200 akawauliza je, huo ndio uongozi?

Lowassa aliwahoji tena, wakati Mkapa anaondoka madarakani bei ya mchele ilikuwa shilingi ngapi? Wananchi wakajibu ilikuwa 1,000 leo imefikia shilingi ngapi? Wakajibu 2,500.

“Naweza kutaja vitu vingine vingi, niridhike kwa kusema nachukia umasikini, nauchukia umasikini kwa akili yangu yote na ndiyo maana naomba ridhaa kwa Watanzania niende Ikulu nikatoe umasikini kwa Watanzania ili waweze kula milo mitatu, wawe na nyumba na gari la kutembelea,” alisema.

“Kwa miaka 50 Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alizungumzia kuhusu umasikini hadi leo bado tunazungumzia suala la umasikini, maradhi na ujinga kwanini? Kwanini tunakubali kuendelea kuwa nyuma, inabidi tufike mahali tujiulize kwanini Waganda, Wakenya, Wanyarwanda watupite kwa uchumi.

Maandamano

Katika maandamano yanayotarajiwa kufanyika leo, Lowassa alitoa wito kwa wanachama wanaounda Ukawa kuwa watulivu katika maandamano watakayofanya kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya kugombea urais.

Maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia katika ofisi za chama hicho na kwenda ofisi za Chama cha NCCR- Mageuzi na baadaye NEC kuchukua fomu na wakishachukua wanamalizia ofisi za Chadema ambapo viongozi wa Ukawa watazungumza na wananchi.

“Kumbukeni maadui zenu huwa wanasema chama chetu kina fujo eti hakina heshima kwa akina mama na wazee, hivyo naomba tujihadhari na maneno hayo na katika maandamano ya leo tuwe na nidhamu na waungwana na tusikilize maelekezo ya Serikali, hawa wanataka kutuzingua hivyo tusiwaruhusu watuzingue,” alisema.

“Kwa kupitia umoja wetu tujue kwamba tusipochukua Ikulu mwaka huu itatuchukua miaka 50 ijayo, hivyo nawapeni pole kwa kujiuzulu kwa mwenyekiti wenu,” alisema.

“Ukawa kuna viongozi hodari na imara kwani wamepitia misukosuko mingi sana, lakini wameishinda kwa umoja na mshikamano wangeyumba wangechukulia poa.

“Ukawa ina Mwenyekiti wake, Emanuel Makaidi, Mwenyekiti Freeman Mbowe, James Mbatia ambaye anajua Qur’an na Biblia na Maalim Seif ni hodari sana wa kupatanisha watu na ni mpambanaji asiyekata tamaa nimepata faraja kujiunga nao,” alisema.

POLE YA KUONDOKA LIPUMBA

Lowassa pia alitoa pole kwa wanachama wa CUF kwa kuondokewa na mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, ikiwamo na kuwapongeza kwa namna walivyolikabili jambo hilo.

“Tatizo la Afrika viongozi wanatumia mamlaka kienyeji sana, wamekuwa wanatengeneza Katiba kwa kuwarejesha madarakani ila hapa tunachotakiwa kufanya ni kuendelea kushirikiana na kuwa na umoja,” alisema.

Alisema mwaka 1995, Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Nyerere alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM aliwaambia wanachama wa chama hicho kwamba, ‘watu wengi wanataka mabadiliko hivyo wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM’.

Baada ya kusema maneno hayo, Lowassa alitoa kauli mbiu yake inayosema ‘safari ya mabadiliko wananchi wakajibu ‘nje ya CCM’.

Alisema ujio wake Ukawa, ni kutekeleza maagizo ya Mwalimu Nyerere ya kumtaka kutafuta mabadiliko nje ya CCM ikiwamo na kuandika historia ya nchi ambayo inawezekana.

“Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuli…wasiwadanganye kwani tupo imara na Mwenyezi Mungu atatusaidia, kwani wanajaribu kupitisha fedha lakini wajue kuwa viongozi wa Ukawa hawahongeki,” alisema.

MTANZANIA

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Mkoa huo, Isack Joseph, wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha  Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ole Nangole na Joseph walifikia uamuzi huo jijini hapa jana na kusema kwa nyakati tofauti wamelazimika kuchukua uamuzi huo kwa kuwa utaratibu wa kumpata mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulikiukwa.

Kwa mujibu wa wana CCM hao, wakati wa mchakato huo baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho walikuwa na wagombea wao mifukoni waliotaka wagombee nafasi hiyo.

Kwa upande wake, Ole Nangole aliyejiondoa CCM akiwa kwenye kipindi cha awamu ya pili cha uenyekiti wake, alisema alijiunga CCM mwaka 1977 ambapo alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo mwenyekiti wa CCM wilaya kwa miaka kumi.

“Ndugu zangu waandishi wa habari nimewaita leo kuwaambia jambo moja kwamba ninahama CCM kuanzia sasa. Najiuzulu nafasi yangu ya mwenyekiti niliyoitumikia kwa miaka saba na ninajiunga na Chadema kuanzia sasa.

“Nashindwa kuwa na moyo wa chuma wa kuendelea kuwa ndani ya CCM kwa sababu CCM niliyoifahamu tangu enzi za TANU siyo hii ya sasa.

“Kuondoka kwangu kumechangiwa na kikundi cha viongozi wachache kuiongoza CCM kwa mabavu, nguvu na kwa kutumia fedha walizokwapua serikalini.

“Miaka yote tangu nilipojiunga CCM mwaka 1977, sikuwahi kukiona chama hiki kikiendesha mambo yake bila kufuata kanuni na taratibu za vikao kama kilivyofanya wakati wa vikao vya kupitisha mgombea urais mjini Dodoma hivi karibuni.

“Mkutano mkuu wa CCM uliongozwa kwa kukiuka haki na misingi kwa wanachama kwani hata nyinyi mtakumbuka kulikuwa na mchakato wa urais na wagombea 40 walijitokeza akiwamo Edward Lowassa.

“Kwa mapenzi yake Lowassa alivyokitumikia chama na Taifa, wananchi tuliamini mchakato ule kama jina lake lisingekatwa angekuwa mmoja wa wagombea ambao wangefika mbali ndani ya chama.

“Lakini jina lake lilikatwa bila sababu japokuwa sababu tulizijua tangu alipotoka kwenye uwaziri mkuu kwa vile kuliendelea kusambazwa maneno na hujuma za kisiasa dhidi yake kupitia kwa viongozi wa chama na Serikali wakiwamo vijana wadogo waliopewa fedha na madaraka ili wamchafue,” alisema Ole Nangole.

Kwa upande wake, Joseph alimnyooshea kidole Katibu wa CCM, Abdulrahman Kinana na kumtaka achunge ulimi wake pindi anapowaita Watanzania makapi ndani ya nchi yao.

Joseph ambaye ni Diwani wa Kata ya Monduli Mjini aliyemaliza muda wake na kupita bila kupingwa ndani ya CCM, alisema hakuna Mtanzania aliye makapi kwani wote wana haki ya kidemokrasia ya kuhama vyama kwa jinsi watakavyoona inafaa.

“Watasema mengi na tumeondoka watatuita makapi. Naomba niwaambie, sisi siyo makapi, wakitaka tuzungumze suala la makapi hao wanaosema hivyo wao ndio makapi halisi.

“Sisi Watanzania si makapi kwani tukichambuana kwa suala la makapi na kuangalia wewe umetokea wapi, tutakwenda kusiko. Kwanza aliyesema hiyo kauli yeye ni Msomali. Hivyo tukisema nani ni makapi yeye ndiye makapi halisi anayeishi Tanzania kwani asili yake ni Somalia,” alisema Joseph.

Joseph alitoa kauli hiyo zikiwa ni siku chache baada ya Kinana kunukuliwa na vyombo vya habari akisema wanachama wa CCM wanaohamia Chadema ni makapi.

Akizungumzia kuhusu kuhama kwake, alisema ametafakari kwa muda kilichotokea mjini Dodoma na kisha kuamua kuiridhisha roho na nafsi yake, kwamba kilichofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM kilikuwa ni uhuni wa kisiasa.

“Mheshimiwa Lowassa alisema demokrasia imebakwa ndani ya CCM. Mimi nasema kanuni na taratibu za CCM zimehodhiwa na kikundi cha watu wachache.

“Ukiona wachache wanahodhi madaraka ya chama, huna sababu ya kurudi nyuma na kuangalia chama ni cha watu wachache au ni cha wanachama.

“Hivyo basi, nimetafakari kwa muda mrefu, nimeridhika kwamba uamuzi ninaouchukua kuondoka CCM na kujiunga na Chadema ni sahihi,” alisema Joseph.

MTANZANIA

JOTO la uteuzi wa mwisho la kupata wagombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) limezidi kupanda, huku chama hicho kikitangaza uamuzi mgumu kwa wagombea waliocheza rafu na hata kupindua matokeo.

Mbali na hayo, viongozi wa ngazi ya wilaya na mikoa wanaodaiwa kuwabeba kinyume na utaratibu nao wapo hatarini kuvuliwa nyadhifa zao.

Taarifa kutoka ndani ya CCM zililiambia MTANZANIA jana kuwa kikao cha Sekretarieti kilichokutana mjini hapa, kilijadili baadhi ya taarifa na rufaa za wagombea, huku wengine wakiwalalamikia wenzao pamoja na viongozi kwa kucheza rafu wakati wa uchaguzi wa kura za maoni.

Miongoni mwa jambo ambalo limekuwa likizua mjadala, ni hatua ya baadhi ya wabunge kupata kura nyingi katika maeneo yao kinyume na idadi halisi ya wanachama wa CCM kwenye jimbo husika.

Moja kati ya majimbo ambayo wagombea walilalamikia hatua hiyo, ni Jimbo la Iramba ambapo Juma Kilimbah ambaye alikuwa ni moja ya wagombea, alisema pamoja na kura kupigwa bado kura alizopata mgombea mwenzao, Mwigulu Nchemba ni tofauti na idadi ya wapiga kura.

Alidai wakati wa mchakato huo, baadhi ya viongozi wa CCM akiwemo msimamizi wa uchaguzi, walikuwa wakigawa kadi kinyume na utaratibu kwa lengo la kumwezesha Mwigulu kushinda.

Akizungumza mjini hapa, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema vikao hivyo vilivyoanza jana vinaweza kutengua ushindi wa wagombea hao.

Alisema wamepokea malalamiko mengi kuhusu ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi katika upigaji wa kura za maoni.

“Pamoja na uchaguzi kumalizika ni lazima wana CCM watambue kuwa kulalamika pembeni au katika vyombo vya habari hakusaidii, ni lazima wafuate utaratibu wa chama.

“Kikubwa wanachama wawe watulivu na vikao hivi vitachambua kwa kina kila tukio katika kila jimbo, wilaya na hata mkoa kabla ya kuteua jina la mgombea wa ubunge kwenye jimbo husika,” alisema Nape.

NIPASHE

Baada kimya cha muda mrefu hatimaye Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilibrod Slaa, anatarajiwa kufungua pazia la kampeni za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Imeelezwa kuwa, Dk. Slaa ambaye kwa sasa amepewa likizo na chama chake baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiunga na chama hicho, atafungua kampeni za Ukawa mkoani Dar es Salaam mwezi huu.

Kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zitaanza rasmi Agosti 22, mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chadema, John Mnyika, alidokeza kwamba Dk. Slaa atazindua kampeni za Ukawa katika Jimbo la Kibamba, ambalo yeye (Mnyika) anagombea ubunge kwa tiketi ya umoja huo.

Mnyika alidokeza hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na viongozi wa matawi na kata ya Goba, muda mfupi kabla ya kufanyika uchaguzi wa kura za maoni kumchagua mgombea udiwani katika eneo hilo.

“Dk. Slaa yupo mapumzikoni na jana nilizungumza naye kwa kirefu na aliniambia bado anapumzika, lakini atakuja kushiriki kampeni Jimbo la Kibamba ambalo mimi nagombea ubunge,” alisema Mnyika.

Hata hivyo, Mnyika alipoulizwa kama Dk. Slaa atashiriki kampeni za nchi nzima ama ataishia Jimbo la Kibamba pekee kama alivyozungumza naye, Mnyika hakutaka kufafanua zaidi.

Katibu huyo wa Chadema hajashiriki katika shughuli mbalimbali za Ukawa ikiwamo kikao cha Ukawa cha kumkaribisha Lowassa kwenye makao makuu ya Chama cha Wananchi (Cuf), mapokezi ya mwanasiasa huyo na mkutano mkuu wa Chadema uliompitisha kugombea urais kupitia Ukawa.

Hata jana Dk. Slaa hakuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Taifa la Cuf ambao ulihudhuriwa na viongozi wote wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD.

Waliohudhuria jana ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi.

Pia walikuwapo wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad na mgombea mwenza, Juma Haji Duni.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa Chadema wiki iliyopita, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, Dk. Slaa kwa sasa yupo mapumzikoni, lakini kampeni zitakapoanza ataongoza kampeni za Ukawa  kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwa ngazi ya udiwani, ubunge na urais.

Mnyika aliwaeleza wananchi wa kata hiyo kuwa Ukawa utashinda uchaguzi huu na kwamba kinachotakiwa ni wao kujiandaa kufanya kampeni za nguvu ili kuwafikia wananchi wengi.

Hata hivyo, Dk. Slaa alipotafutwa jana kuthibitisha maelezo ya Mnyika, simu yake ya mkononi haikupatikana.

Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.

Katika kura za maoni kata ya Goba, viongozi wa matawi na kata walimchagua, Rick Ambinga, kupeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi ya udiwani.

Ambinga aliwashinda wagombea wenzake wanne katika uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na Katibu wa Jimbo la Ubungo, Justin Mollel.

Habari za Dk. Slaa kuzindua kampeni za Ukawa kama zitakuwa ni za kweli itakuwa faraja kwa wafuasi na viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa.

Wiki iliyopita zilivumishwa taarifa za uvumi zikidai kuwa kiongozi huyo angerejea katika ofisi za Chadema kuendelea kuchapa kazi, hali iliyowalazimisha baadhi ya wafuasi wa Chadema kwenda katika ofisi hizo, lakini walielezwa na viongozi kuwa hazikuwa habari za kweli.

Alhamisi iliyopita, Ukawa ilipata mtikisiko, baada ya Mwenyekiti wa Cuf, Prof. Ibrahim Lipumba, kutangaza kujiuzulu akidai kuwa amechukua uamuzi huo kutokana na kuonekana kuwa kikwazo katika baadhi ya mambo ndani ya Cuf na kwamba roho yake imemsuta asikubaliane na uamuzi wa Ukawa wa kumpokea Lowasa na kumpa fursa ya kugombea urais kupitia Ukawa.

HABARILEO

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa amekanusha uvumi kuwa ameungana na wenyeviti wengine wa mikoa wa CCM kukihama chama tawala nchini. Amesema wanaomzushia washindwe na walegee, kwani moyo na mwili wake upo CCM na kwamba kamwe hawezi kuhama.

Aliyasema hayo jana mjini hapa kutokana na kuwapo kwa taarifa amekihama chama hicho. Awali, jana kulikuwa na taarifa za Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole kuhamia Chadema, kama ilivyokuwa kwa Mgana Msindai, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida aliyetangulia Chadema wiki iliyopita baada ya kushindwa kura za maoni ndani ya CCM.

Katika kuthibitisha hayo, Kimbisa jana alikuwa akiendesha vikao vya Kamati ya Siasa ya Mkoa akiwa katika sare zake za chama. Taarifa hizo zimekuja huku Kimbisa akiwa na habari nyingine katika gazeti hili (ukurasa wa 21) akielezea kushangazwa na wanaokihama chama baada ya kushindwa katika michakato ya kuwania uongozi, huku akisema kamwe yeye hawezi kufanya hivyo.

“Mwaka 2010 niligombea ubunge Jimbo la Dodoma Mjini nikahesabu kura zangu mwenyewe nyumbani nikajiona nimeshinda nikalala, asubuhi nilipoamka kumbe wagombea wenzangu wakaunganisha matokeo yao mgombea mmoja akaonekana ameshinda, lakini bado sikuhama na hadi leo nina damu ya kijani.

“Mtu akihangaika kuondoka CCM baada ya kushindwa tutamfuata hukohuko na tutampiga kwa kura tu,” alisisitiza Kimbisa.

HABARILEO

Huku akikaribia kukabidhi madaraka kwa Rais wa Awamu ya Tano baadaye mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete amesema moja ya sifa yake na ya chama tawala, CCM, ni kutekeleza ahadi walizowaahidi Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010.

Amesema ahadi nyingi alizowaahidi wananchi ambazo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, zimetekelezwa. Aidha, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema utawala wa Rais Kikwete umekuwa na mafanikio makubwa kwenye sekta ya ujenzi.

Amesema katika kipindi cha miaka 10, serikali imenunua vivuko vipya 15 na kukarabati vivuko saba na kwamba hayo yote yamefanikiwa kwa kuwa Watanzania walimuamini Rais Kikwete na kumpa nafasi ya kutekeleza ahadi kwa vitendo. Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizindua kivuko cha Mv Mafanikio kinachofanya safari zake kati ya Mtwara na Msangamkuu.

Alisema wakati wa kampeni mwaka 2010, aliwaahidi wananchi wa Msangamkuu kuwapatia kivuko ambapo ahadi hiyo imetekelezwa. “Hiyo ndio sifa yangu pamoja na chama chetu, tunapoahidi tunatekeleza kwa vitendo na leo hii wananchi wa Msangamkuu wameondokewa na kero ya usafiri waliokuwa wanapata,” alisema.

Alisema kivuko hicho ni fursa nzuri kwa kukuza uchumi wa wananchi na amewataka waitumie vizuri fursa hiyo. Rais Kikwete alisema wananchi wa Msangamkuu walikuwa wanapata shida ya usafiri na kwamba walikuwa wanalazimika kuzunguka umbali wa kilomita 21 hadi kufika Mtwara mjini, hivyo adha hiyo kwa sasa itakuwa historia.

Kwa upande wake, Dk Magufuli alisema katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Rais Kikwete amefanikiwa kununua vivuko vipya 15 na kukarabati saba ambavyo hivi sasa vinafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Alisema tangu serikali ya awamu ya kwanza mpaka serikali ya awamu ya tatu, kulikuwa na vivuko 13 na kwamba hivi sasa vipo zaidi ya 28. “Hatuna budi kukushukuru Mheshimiwa Rais kwa kuboresha huduma mbalimbali za usafiri, utawala wako umeweza kununua vivuko vipya 15 na kukarabati saba hilo si jambo dogo, tunakushukuru sana na rais ajae ataendeleza zaidi ya hapo ulipoishia,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliojitokeza.

Alisema kivuko hicho kimegharimu Sh bilioni 3.3, ambazo zimetolewa na serikali. Dk Magufuli ambaye ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, alisema wanafunzi na walemavu watavuka bure katika kivuko hicho na kwamba watu wazima watalipia Sh 300, watoto Sh 100.

Dk Magufuli alisema Rais Kikwete aliahidi barabara kutoka Dar es Salaam mpaka Mtwara ambayo hivi sasa imekamilika. “Watanzania wana kila sababu ya kukushukuru Rais Kikwete umewafanyia mambo mengi, wewe ni kiongozi mwenye upendo, imani na kubwa zaidi umetekeleza kwa vitendo uliyoahidi,” alisema.

Aidha alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi kuwa ndiye mgombea urais wa CCM. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Marcelin Magessa, alisema mkoa wa Mtwara kuna vivuko viwili kikiwemo cha Mv Kilambo na Mv Mafanikio.

Alisema kivuko cha Mv Mafanikio kilitengenezwa na mkandarasi wa hapa nchini na kwamba kilianza kutoa huduma mwaka jana. Alisema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 50 na magari matatu kwa wakati mmoja.

Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, alisema wananchi walikuwa wakipata shida ya usafi ambapo baadhi yao walipoteza maisha kutokana na kukosa usafiri wa uhakika. Alisema ujenzi wa kivuko hicho unatokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Dk Magufuli na kwamba wananchi wa jimbo hilo wanampongeza.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu, alisema kata ya Msangamkuu ina wakazi zaidi ya 1,200, ambapo kivuko hicho ni mkombozi mkubwa kwa wakazi hao. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe, wabunge na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi.

HABARILEO

Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vingine vitatu vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amewapa pole wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa mshituko wa kuondokewa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu, huku akiwataka kutovunjika moyo, bali waongeze mshikamano ili dhamira ya kuingia Ikulu iweze kutimia.

Aidha, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ameonya kuwa, hawatamvumilia yeyote atakayeonekana kutaka kukwamisha umoja wao unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Akizungumza na wananchi waliofika kumpokea alipotembelea ofisi za CUF Buguruni, Dar es Salaam jana ambako pia alihudhuria kikao cha Baraza Kuu la CUF, Lowassa aliwapa pole wanaCUF akisema endapo watatetereka, safari yao ya kuelekea Ikulu itakuwa ngumu.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba wafuasi wa CUF kumsindikiza kwa wingi leo kwenda ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya kuwania urais baadaye mwaka huu, huku akisisitiza ana imani ya kushinda.

Awali, mgombea mwenza wa Lowassa, Juma Duni Haji ambaye alijiunga Chadema hivi karibuni akitokea CUF alikokuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Taifa, alisema endapo wanachama wa vyama vinavyounda Ukawa watakosea katika kupiga kura zao na kushindwa kuingia madarakani, basi watalazimika kusubiri miaka 50 ijayo ili kuingia Ikulu.

“Tusipoweza kuingia Ikulu sasa litakuwa kosa kubwa na itatulazimu kusubiri miaka 50 ijayo ili kuweza kuchukua madaraka. Vijana pekee ndio watakaoweza kuleta mabadiliko,” alisema Duni.

Akizungumzia shughuli ya kuchukua fomu leo, Lowassa aliwataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kumsindikiza na kusisitiza kuwa amejiunga na Ukawa ili kutafuta mabadiliko nje ya CCM na kuwa ana imani ya kushinda kwa asilimia 90.

Lowassa alisema endapo Ukawa itashinda na kuchukua madaraka wataendesha nchi kwa utulivu na kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kuwaondolea umasikini ambao umekuwa ukipigwa vita tangu mwaka 1962. Naye Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema kiongozi ndani ya Ukawa ambaye atakuwa akipingana na malengo yao kutokana na kukosa fursa binafsi, mtu huyo hafai kuwa katika umoja huo.

Alisema pamoja na umoja huo kukumbwa na misukosuko, bado wamekuwa wamoja na kutetea hatua ya wao kumteua Lowassa ambaye wiki mbili zilizopita alikuwa CCM kwa sababu ni Mtanzania. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema silaha pekee ya ushindi kwa Ukawa ni kuwa na umoja, ushirikiano na mshikamano na kuwa ana uhakika Lowassa atashinda, sambamba na yeye kwa upande wa Zanzibar.

“Lowassa ni rais anayesubiriwa kuapishwa, na Zanzibar kuna mtu anaitwa Maalim Seif ameshamaliza kazi naye anasubiri kuapishwa,” alisema na kuongeza kuwa amefarijika kwa Lowassa kutembelea CUF, jambo ambalo linadhihirisha umoja wao.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia alisema Ukawa haitahubiri siasa za chuki ili uchaguzi ufanyike kwa amani na kuwaonya viongozi wa CCM kuchunga ndimi zao. Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema watakaoiondoa CCM madarakani ni wananchi wenyewe kwa kujitokeza kupiga kura.

Lowassa leo atachukua fomu ya uteuzi wa urais katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akiambatana na mgombea mwenza Duni. Msafara wa kumsindikiza Lowassa, utaanzia Makao Makuu ya CUF, Buguruni asubuhi saa 2:00 na kupitia Makao Makuu ya NCCRMageuzi na baadaye kwenda NEC ambapo saa 5:00 asubuhi mgombea huyo atachukua fomu.

Baada ya kuchukua fomu, Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa ya kuiingiza Serikali katika mkataba wa kufua umeme wa kampuni feki ya Richmond na baadaye kuchujwa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM, atakwenda Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni.

Wakati huohuo, Emmanuel Ghula anaripoti kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kimechagua kamati ya watu watatu ambao watafanya kazi zilizokuwa zikifanywa na Mwenyekiti wa chama hicho aliyejiuzulu, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na makamu wake, Juma Duni Haji.

Walioteuliwa ni Twaha Taslima ambaye atakuwa mwenyekiti wa kamati, Abubakar Khamis na Severina Mwijage. Kuundwa kwa kamati hiyo kunatokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba huku makamu mwenyekiti wake kujiunga na Chadema kama mgombea mwenza wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).


Akitangaza uamuzi wa baraza kuu la uongozi wa taifa wa chama hicho, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema kuwa chama hakiwezi kukaa kwa kipindi cha miezi sita bila kuwa na mwenyekiti wala makamu wake, wameamua kuteua kamati ya watu watatu kama ambavyo katiba yao inawataka.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment