Monday, 10 August 2015

CCM MKOA WA IRINGA YAMALIZA UTEUZI WA WAGOMBEA UDIWANI, MWENYEKITI WA CCM MUFINDI AKATWA


HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa imefanya uteuzi wa wagombea udiwani katika kata za majimbo yote huku ikithibitisha kumkata Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mufindi, Yohanes Kaguo.

Kaguo aliyekuwa diwani wa Kata ya Makungu wilayani Mufindi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita amekatwa baada ya kushindwa kura za maoni za kata hiyo.

Katika kura hizo za maoni, Kaguo anayeelekea kupotoza ushawishi ndani ya chama hicho alipata kura 351 dhidi ya kura 465 alizopata Kizito Kambo.

“Kwa matokeo hayo halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Iringa inampendekeza Kizito Kambo kuwa mgombea udiwani katika kata hiyo,” alisema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu huku wajumbe wengine wakiafiki uteuzi huo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi anayemaliza muda wake, Peter Tweve alinusurika kukatwa katika kikao hicho kichofanye uteuzi wa wagombea wa kata 37 za wilaya ya Mufindi baada ya mmoja wa wajumbe kuingiza hoja inayomuhusisha na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.

Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho (hakutaja jina) alisema Tweve aliyeshinda kwa mara nyingine tena kura za maoni za kata yake ya Kiyowela anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa alimuokoa diwani huyo akisema; “hatuwezi kumuhukumu mtu kwa tuhuma, tumesikia tuhuma hizo na kama bado zipo atawajibika kwa nafasi yake, hatuwezi kufanyia kazi tuhuma mpaka mtu ahukumiwe.”

Katika jimbo la Iringa Mjini wagombea wa kata 18 waliteuliwa akiwemo Farida Mpogole wa kata ya Mtwivila ambaye viongozi wa CCM Iringa Mjini walimrushia tuhuma zinazomuhusisha kuwa na mahusiano ya jirani na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa.

Mwingine aliyepitishwa Iringa Mjini ni Benjamini Chatanda wa kata ya Igumbilo anayehusishwa na tuhuma za udanganyifu na matumizi ya fedha wakati wa kura hizo za maoni.

Pamoja na kuteua wagombea udiwani wa wilaya ya Mufindi na Iringa Mjini, kikao hicho pia kiliteua wagombea wa kata 28 wa Iringa Vijijini na 24 wa wilaya ya Kilolo.

Baaada ya hitimisho la uteuzi huo, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa alisema; “tuna kazi kubwa mbele yetu, ule wimbo wetu wa wataisoma namba ili uwe kweli ni lazima tujipange, vinginevyo tunaweza kuwa sisi CCM wa kusoma namba za watu, turudi tukajipange.”

Alisema ni jukumu la viongozi kuhakikisha wanarekebisha hali ya hewa kwa kusaidia kuvunja makundi, kama yapo, ili katika mchakato wa uchaguzi huo waende pamoja.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment